Tanzania yazidi kuporomoka FIFA

Taifa Stars
LICHA ya kuambulia sare ya 1-1 ugenini na Namibia mwezi uliopita, Tanzania imezidi kuporomoka kwenye orodha ya viwango vya soka vya FIFA baada ya kushuka kwa nafasi tano toka nafasi yake ya awali.
Kwa mujibu wa orodha mpya ya FIFA, Tanzania sasa imeporomoka hadi nafasi ya 122 toka 117 iliyokuwa inaishikilia katika orodha ya Machi ikiwa nyuma ya Malawi iliyo katika nafasi ya 121.
Pia imeizidi kidogo tu nchi iliyo kwenye vita vya muda mrefu Afghanistan waliopo kwenye nafasi ya 123 ambayo haina mvuto mkubwa katika soka.
Nchi zilizo chini ya Tanzania ambazo zinatokea Afrika Mashariki na Kati ni Burundi iliyo katika nafasi ya 125 baada ya kupanda nafasi nne, wakati Rwanda iko namba 129 baada ya kukwea nafasi tano juu.
Kenya iko katika nafasi ya 106 baada ya kupanda nafasi tatu, Sudan nafasi ya 117, Ethiopia wanashika 101 wakati Waganda ndiyo wanaonekana vinara katika ukanda huu kwa kuwa wako 86 huku wakiwa wameporomoka nafasi moja tu.
Katika orodha ya Dunia, Hispania imeendelea kuongoza ikifuatiwa na Ujerumani, Ureno ikiwa nafasi ya tatu na kufuatiwa na Colombia, Uruguay na Argentina wakati wenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia, Brazili wanakamata nafasi ya sita kisha Uswisi, Italia na Ugiriki imefunga dimba la 10 Bora.

Post a Comment

أحدث أقدم