Uchunguzi
huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo kujenga
dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara
kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na
Serikali.PICHA|MAKTABA
Ongezeko la
kasi ya ujangili nchini limedaiwa kusababishwa na vitendo vya rushwa,
matumizi mabaya ya madaraka na mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria
katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopewa jina la Urasimishaji wa Ujangili wa
Kitaalamu Afrika, tangu mwaka 2000 wizara hiyo imejikuta katika kashfa
za rushwa na kusababisha mawaziri na watendaji wakuu kuvuliwa nyadhifa
zao.
Katika ripoti hiyo, Taasisi ya Kimarekani ya Utunzaji Wanyamapori ya
Born Free USA kwa ushirikiano na Shirika la Ripoti za Kichambuzi na
Takwimu la C4ADS, imeeleza pia jinsi vikundi vya waasi barani Afrika
wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi huu nchini Kenya, inaitaja Tanzania
kama kitovu cha kusafirisha pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika
Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikishindana na ile ya
Mombasa katika kutumia bandari kibiashara.
Kutoka mwaka 2008 mpaka 2013, inaelezwa zaidi ya tani 20 za pembe za
ndovu ama zilikamatwa zikisafirishwa kuingia au kutolewa katika Jiji la
Dar es Salaam, hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya C4ADS.
Ripoti hiyo
inafafanua kuwa uchunguzi wa vinasaba (DNA), katika tani 11 za pembe za
ndovu zilizokamatwa Taiwan, Japan na Hong Kong mwaka 2006, ilibainika
kuwa pembe 1,500 zilitoka Tanzania (Selous).
Uchunguzi
huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe hizo vilifanana, hivyo kujenga
dhana kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakiwinda katika hifadhi hiyo mara
kwa mara katika utaratibu maalumu unaotambuliwa na Serikali.
“Kuna
udhaifu mkubwa katika usimamizi wa uwindaji halali na wawindaji wenye
vibali hawasimamiwi ipasavyo kufanya uwindaji kwa taratibu zilizowekwa
kisheria. Hivyo hutumia nafasi hiyo kufanya vitendo vya ujangili,”
inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Serikali yakanusha
Hata hivyo,
Mkurugenzi wa Wanyamapori, Paul Sarakikya alikanusha madai hayo akisema
siyo kweli kwamba wawindaji halali huachwa bila usimamizi, bali wana
mifumo ya kusimamia shughuli hiyo.
“Sikubaliani
na ripoti hiyo, tumeshaongea sana juu ya suala hili, Rais
alishalizungumzia na waziri pia. Ufafanuzi ndio huo, hamna ukweli wowote
katika ripoti hiyo,” alisisitiza Sarakikya.
Salakikya alisema idadi ya tembo nchini inazidi kuongezeka katika hifadhi tofauti na upungufu unaoelezwa katika ripoti hiyo.
Mkurugenzi
huyo alihoji kuwa kama hakuna usimamizi madhubuti katika uwindaji
halali, wamewezaje kusimamia uwindaji miaka yote mpaka idadi ya tembo
inaongezeka, baada ya upungufu uliokuwepo miaka ya nyuma.
Wakati
Sarakikya akisema tembo wanaongezeka, ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi ya
tembo katika hifadhi za Selous na Mikumi kwa mwaka 1976, ilikuwa ni
109,419 lakini kufikia mwaka 2009, idadi hiyo ilishuka hadi kufikia
tembo 38,975.
Nchi
zilizoathirika zaidi na ujangili barani Afrika, zinatajwa kuwa ni
Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Cameroon, Msumbiji, Kenya, Zimbabwe na Tanzania ambayo pia inatajwa kuwa
kitovu cha usafirishaji wa pembe za ndovu.
Idadi ya tembo waliosalia
Na kwa
utafiti uliofanywa na Taasisi ya Frankfurt Zoological Society mwishoni
mwa mwaka 2013, ripoti hiyo inaeleza kuwa ni tembo 13,084 wanaokadiriwa
kusalia katika hifadhi, sawa na upungufu wa asilimia 66 katika kipindi
cha miaka minne tangu 2009.
Hii
imefafanuliwa kuwa zaidi ya tembo 25,000 waliuawa katika Hifadhi ya
Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia, ripoti hiyo inabainisha upungufu
wa tembo katika hifadhi ya Ruaha-Rungwa kutoka tembo 35,461 mpaka tembo
20,090 sawa na upungufu wa asilimia 36.5 kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa.
Post a Comment