MAMBO sasa yameanza kuwa mazuri katika Klabu ya Simba! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na baadhi ya matajiri wenye mapenzi na klabu hiyo ambao walikuwa wamekaa pembeni kwa muda mrefu, kuamua kurudi na kuisapoti ili heshima yake iliyopotea kwa muda mrefu irudi.
Matajiri hao waliikimbia timu hiyo baada uongozi wa sasa unaomaliza muda wake hivi karibuni uliopo chini ya mwenyekiti, Ismail Aden Rage kuingia madarakani.
Mmoja wa matajiri hao ambaye ni Azim Dewji, aliliambia Championi Jumatano kuwa sababu kubwa iliyowafanya waingie mitini kuisapoti timu hiyo ni kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wa uongozi huo ambao alidai kuwa haukuwa na lengo la kuiletea maendeleo klabu hiyo, zaidi ya kujinufaisha wenyewe.
Alisema hivi sasa wameamua kurejea kwa nguvu zao zote na kuisapoti timu hiyo kwa hali na mali ili iweze kurudisha heshima yake iliyopotea kwa muda mrefu.
“Sababu kubwa iliyotufanya turudi kuiunga mkono Simba ni kutokana na kuwa na imani na wagombea wa sasa wa nafasi ya urais wa klabu yetu ambao ni Evans Aveva na Andrew Tupa.
“Uongozi wa Rage tulishindwa kufanya nao kazi kwa sababu hatukuwa na imani nao, ndiyo maana mambo hayakuwa mazuri, hivyo kwa sasa tutahakikisha tunashirikiana vilivyo na kiongozi yeyote atakayeingia madarakani ili kurudisha heshima yetu,” alisema Dewji.
Post a Comment