Yanga yamkomalia Kipre Tchetche

Mshambuliaji wa Azam, Kipre Tchetche.

LICHA ya uongozi wa Azam FC kueleza kuwa haupo tayari kumwachia mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche kwenda Yanga, uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani haujakata tamaa na sasa unapanga mashambulizi upya ili kumsajili straika huyo.
Tchetche ni mmoja wa wachezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha Azam ambacho msimu uliomalizika hivi karibuni, kilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara huku mchezaji huyo akiwa kinara wa mabao.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, uongozi wa klabu hiyo upo katika mikakati kabambe na kubwa zaidi ni kuwa wanasubiri Kipre abakize miezi sita katika mkataba wake na Azam ambapo wanajua watampata kirahisi tofauti na sasa.
“Mpango wetu wa kumsajili Kipre Tchetche upo palepale, hata Azam wabane vipi lazima tutamsajili tu kwa njia yoyote ile na mikakati inaendelea.
“Hata hivyo kwa sasa tumeshapata moja ya njia ambazo tutazitumia ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, kuna watu wake wa karibu tumewapatia jukumu hilo na wametuhakikishia kuwa litafanikiwa tu, hivyo tusiwe na wasiwasi.
“Tunatambua kuwa Azam watahakikisha wanafanya kila jambo ili waweze kumzuia asijiunge na sisi lakini ni matumaini yetu kuwa hawataweza, watu hao tunaowatumia kumshawishi Kipre wana ushawishi mkubwa sana kwake pamoja na kwa wakala wake,” kilisema chanzo hicho.
Walipotafutwa viongozi wa juu wa Yanga, hawakuwa tayari kulizungumzia suala hilo. Yanga wanajua wakimsajili sasa watalazimika kulipa fedha nyingi za usajili lakini kama wakifanya naye mazungumzo miezi sita kabla ya mkataba wake, maana yake ni kuwa kuna uwezekano wa kumsajili na Azam kutopata kitu.
- Champion

Post a Comment

أحدث أقدم