Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Na Ojuku Abraham MOTO wa ripoti
ya upotevu wa fedha za umma katika akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo
imekabidhiwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
inayoongozwa na Zitto Kabwe unatarajiwa kuwaka Novemba 27, mwaka huu,
siku ambayo itasomwa na kujadiliwa bungeni baada ya Mwanasheria Mkuu wa
serikali na vigogo wengine kadhaa kuhojiwa.
Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) ilichotwa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi bilioni 300 katika
hali isiyofahamika na wabunge wanataka ripoti hiyo iliyokabidhiwa kwa
Kamati na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, iwahoji
wahusika wote kabla ya kuileta bungeni kwa mjadala.
Serikali kupitia kwa mwanasheria mkuu wake, Jaji Fredrick Werema na
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, sambamba na
Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi wamekuwa wakisisitiza kuwa fedha hizo
zilitolewa kwa kuzingatia hukumu ya Mahakama Kuu na kwamba haikuwa ya
umma isipokuwa ni ya kampuni hiyo ya kufua umeme ya PAP.
“Katika hili, wabunge nao wamegawanyika, wapo wanaotetea madudu haya
na wengine hawataki kabisa mchezo. Pale mwanzo ilionekana kama ni ajenda
ya wapinzani, lakini kadiri siku zinavyokwenda, hata wabunge ndani ya
chama tawala nao wanaonekana hawataki mchezo. Watu wamepania sana na
huenda kukawa na mshikemshike mkubwa siku hiyo,” alisema mbunge mmoja wa
CCM aliyekataa jina lake kutajwa.
“Inapofikia wakati wa kushughulikia wizi mkubwa kama huu, hatuna budi
kuweka masilahi ya taifa mbele, hatuwezi kukubali fedha nyingi kama
hizi zinaibwa wakati wananchi wanashindwa kupata mahitaji yao ya msingi
kwa sababu ya ukosefu wa fedha, tunataka wote waliohusika katika jambo
hili wawajibishwe na hatua zaidi za kisheria zichukuliwe,” alisema.
Kwa mara ya kwanza, skendo hiyo ya fedha iliibuliwa bungeni na Mbunge
wa Kigoma Kusini, David Kafulila, akisema ana uthibitisho kwamba fedha
hizo zilikwapuliwa na wajanja wachache, baada ya kuitafsiri kimakosa
hukumu ya Mahakama Kuu chini ya Jaji John Utamwa, kwani hakuna popote
ilipotaja Akaunti ya Escrow, akidai ingawa katika kikao kati ya Tanesco,
IPTL na Wizara ya Nishati na Madini walisema fedha zote za akaunti hiyo
zipewe Kampuni ya PAP.
Vigogo wa serikali wanaotajwa kuhusika katika kashfa hiyo ni Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wake Eliakim
Maswi, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndullu,
Mwanasheria Mkuu Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco,
Felchesmi Mramba.
إرسال تعليق