Hospitali Serikali majanga matupu

Dar na Mikoani. Hakufai. Pengine ni neno linaloweza kuwakilisha uhalisi wa hali ilivyo katika baadhi ya hospitali kadhaa za Serikali nchini, ambako mamia ya wagonjwa wanateseka kutokana na uhaba wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambao umeendelea kuzikumba.
Wengi wa wagonjwa waliohojiwa wanalalamikia kushindwa kumudu gharama za dawa ambazo wanapaswa kuzinunua kwenye maduka wakisema hali hiyo inazifanya afya za Watanzania wengi wenye kipato cha chini wanaozitegemea kuwa shakani.
Gazeti hili katika uchunguzi wake limebaini kuwa, uhaba huo pia umesababisha
hospitali nyingi kuwabana wagonjwa kwa kuwatoza fedha kwa ajili ya huduma, ili kujijengea uwezo wa kununua dawa chache, pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya dharura.
Kwa jumla, hali ilivyo ni tofauti ya matarajio ya wengi kwamba kungekuwa na mabadiliko, hasa baada ya Serikali kutangaza kwamba imekwishalipa sehemu kubwa ya deni ililokuwa ikidaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Hivi karibuni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema wizara yake imeilipa MSD Sh20 bilioni ili kupunguza makali ya uhaba wa dawa. MSD inaidai wizara hiyo zaidi ya Sh90bilioni za ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Jana, Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kwa sababu tayari waziri wangu alishatoa tamko bungeni, kwa hiyo kauli yetu ndiyo hiyohiyo aliyotoa mheshimiwa waziri.”
Sura halisi ya uhaba wa dawa inaonekana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako hali imeendelea kuwa mbaya kwani ukosefu huo wa dawa umesababisha baadhi ya wagonjwa kuzidiwa na wengine kupoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Hospitalini Ocean Road, mwandishi wetu alikutana na mkazi wa Arusha, Ashura Iddi aliyefika kutibiwa na kufuatana naye hadi katika duka alikokwenda kununua dawa alizoandikiwa.
Akisaidiwa na mwandishi huyo, Ashura ambaye amekatwa mkono wake wa kushoto kutokana na saratani ya mkono iliyosambaa hadi kifuani, aliambiwa na mfamasia katika Duka la Biomed lililo karibu na ORCI kuwa dawa zake za mionzi zinagharimu Sh166,000.
Hata hivyo, mgonjwa huyo ambaye alikuwa akikohoa mfululizo kiasi cha kutapika, hakuweza kununua dozi hiyo kwani hakuwa na fedha hivyo kurudi wodini kuendelea kukaa akisubiri siku dawa zitakapofika au kupata fedha.
Ashura amelazwa ORCI tangu Oktoba 27, mwaka huu na anasema hajapata matibabu zaidi ya kupewa dawa za maumivu aina ya diclofenac. “Nimekosa hata dawa ya allergy (mzio) ambayo inauzwa Sh1,000 nimeambiwa hakuna,” alisema Ashura.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post