Kikosi hiki cha Zimamoto hakina msaada, ni mzigo

Katuni
Msiba mkubwa ulitokea jijini Arusha juzi. Maduka 180 ya kuuza vitu mbalimbali kwa watalii yaliyopo eneo la Mount Meru jijini humo yaliteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.
Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 3:00 usiku wakati maduka hayo yakiwa yamefungwa na jadi kufikia jana, hakukuwa na taarifa ya kuokolewa kwa mali yoyote kutoka ndani ya maduka hayo ambayo yako umbali mfupi tu kutoka kwenye makao makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini humo.

NIPASHE tunatoa pole kwa wote walioathirika na tukio hili. Ni wazi kwamba hili ni pigo kubwa kwani kwa namna yoyote ile, litakuwa limeathiri uchumi wa mamia ya watu wanaofanya shughuli zao za kujiingizia kipato kila uchao kwenye eneo hilo. Ni imani yetu kuwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo ungali ukiendelea ili kujua chanzo cha kuzuka kwa moto huo na kisha hatua zaidi kuchukuliwa.

Pamoja na kuwapo kwa majonzi hayo, lipo jambo ambalo sisi limetustua zaidi. Nalo ni taarifa kwamba Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji jijini Arusha kiliwaangusha wananchi kwa kuchelewa kufika eneo la tukio licha ya kwamba wako jirani sana kutoka mahala palipokuwa na moto.

Inaelezwa kuwa jitihada za kutosha kuwaita askari wa kikosi hicho zilifanyika, lakini hakukuwa na uitikiaji mwito huo kwa haraka. Kwa watu wa Jeshi la Zimamoto, kuungua huku kwa makumi ya maduka hakukuonekana kuwa ni tukio la dharura.

Matokeo yake, hata walipofika baadaye sana, hawakuwa na la kufanya. Hawakuwa na maji. Moto ukaendelea kuwaka kwa kasi na kuunguza kila kilichokuwapo. Wananchi wakawa na hasira kali dhidi yao. Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo, naye alishangazwa na ugoigoi ulioonyeshwa na Kikosi cha Zimamoto. Akaungana na wananchi kulalamika, huku akikiri kwamba  wanapaswa kuadhibiwa kwa kushindwa kuonyesha jitihada za dhati za kuzima moto huo.

Hakika, hili ni jambo la kusikitisha. Ni mwendelezo wa matukio mengine kadhaa yanayothibitisha kuwa Kikosi cha Zimamoto hivi sasa hakina msaada unaotarajiwa kwa umma. Kuchelewa sana ndiyo kawaida yao. Kufika wakiwa hawana maji wala vitendea kazi vya kutosha ni jambo lililozoeleka.

Na mbaya zaidi, hata askari wake huwa hawaonekani kuwajibika vyema. Wananchi huishia kulia na kusaga meno wanapoona kuwa hawapati msaada unaotarajiwa kutoka kwa askari wa kikosi hiki.

Kadri tunavyofahamu, suala la fedha siyo kikwazo kikubwa kwao. Ni kwa sababu zipo hatua kadhaa zimechukuliwa kuimarisha jeshi hili ikiwa ni pamoja na kulitengea fedha nyingi zinazotozwa kwa kila gari linalolipiwa leseni kila mwaka kupitia Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA). Zipo pia fedha nyingine nyingi zinazokusanywa kwa ajili ya jeshi hili kupitia huduma yake ya ukaguzi wa majengo.

Ikumbukwe kuwa miji yetu imekuwa ikipanuka kwa kasi kubwa na tena kwa kujengwa kiholela kila uchao. Kwa sababu hiyo, inatarajiwa kuwa Kikosi cha  Zimamoto kinakuwa imara na kuwa tayari wakati wote kwa shughuli ya uokoaji.

Jeshi hili linatarajiwa kuwa na askari wenye ujuzi wa kutosha, kuwa na vifaa vya kisasa vya uokoaji na pia kuwa na watu waliohamasika kwa ajili ya kuutumikia umma.

Hawapaswi kuzidiwa kwa vifaa na uwezo na vikosi vya kampuni binafsi za ulinzi kwani serikali ina nguvu kubwa zaidi, rasilimali kubwa zaidi na hivyo, huduma zake katika eneo hili zinapaswa kuwa za kiwango cha juu zaidi na kuwa mfano kwa wengine.

Haitarajiwi hata kidogo kuona kuwa Kikosi cha Zimamoto kikichelewa kufika katika eneo la tukio kwa wakati. Haitarajiwi vilevile kuona askari wa jeshi hili wakifika eneo la tukio wakiwa na vifaa chakavu na kukosa hata maji ya kuzima moto na hivyo kuishia kuwa waombolezaji.

Ieleweke kuwa kukumbushia yote haya hatumaanishi kwamba askari wa Zimamoto wanapaswa kufanya kazi kama mashujaa wa filamu za watoto zenye matukio ya kufikirika kama 'super man'. Bali, tunataka kuona kuwa jeshi hili likiwajibika na siyo kuwaangusha wananchi kama ilivyotokea juzi Arusha.

Ikibidi, basi kikosi hiki kifumuliwe chote na kusukwa upya ili tupate kikosi kipya kitakachokuwa na wachapakazi wenye kujali maslahi ya umma. Siyo kuwaangusha wananchi kama ilivyotokea juzi jijini Arusha.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم