
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya.
Chama hicho kimesema iwapo dosari hizo hazitarekebishwa, itakuwa ni vigumu kwa uchaguzi huo kufanyika Desemba 14, mwaka huu kama ilivyoelezwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, alisema mwongozo huo unakinzana na kanuni zake na hata walipozibainisha dosari hizo na kuzipeleka kwa Waziri Mkuu na Ofisi ya Tamisemi, alidai zilirudishwa kama zilivyo.
Kwa mujibu wa Sakaya, muda wa kuwasilisha pingamizi kwa msimamizi msaidizi kwenye muongozo huo ni siku nne huku ule wa kamati ya rufaa kusikiliza rufaa ukiwa ni siku nne kuanzia Novemba 26 hadi 29, mwaka huu.
Hata hivyo alisema mwongozo huo hauonyeshi muda wa kusikiliza pingamizi hiyo kwa msimamizi msaidizi wala muda wa kukata rufaa iwapo mgombea hakuridhika na maamuzi ya msimamizi huyo.
Alisema, kwa upande wa mtaa, kanuni inaonyesha kutakuwa na nafasi saba za kugombaniwa huku mwongozo ukitoa ufafanuzi wa nafasi sita na kwamba wilaya za Temeke na llala, wagombea wamepewa fomu za kugombea nafasi sita na ile ya Kinondoni jijini humo,nafasi saba.
Kwa mujibu wa Sakaya maelezo hayo yanapingana na kanuni katika ibara ya 7.1 (a) na (b) inayoeleza kwamba wajumbe wa kamati ya mtaa watakuwa ni mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wasiozidi sita ambao watachaguliwa na wakazi wa mtaa.
Pia katika mwongozo wa ibara ya 10.2 (a), (b) na (c) aambao unaeleza kwamba, kamati ya mtaa itakuwa na wajumbe wasiozidi sita watakaochaguliwa na wakazi wa mtaa.
Alitaja dosari nyingine kuwa ni pamoja na ile iliyopo kwenye kanuni ibara ya 7 (1) ambayo imeshindwa kutoa namba maalumu ya wajumbe halali wa serikali ya kijiji.
Alisema kipengele hicho kinaonyesha kwamba wajumbe wa halmashauri ya kijiji hawatapungua 15 na hawatazidi 25 huku idadi ya wajumbe katika viti maalumu ikitofautiana na mwongozo wake kwani katika ibara hiyo kifungu c, inasema miongoni mwa wajumbe watakaochaguliwa wakiwamo wanawake, idadi yao itakuwa chini ya nusu ya wajumbe wa halmashauri.
Jumanne Sagini, Katibu Mkuu wa Tamisemi, alipotafutwa, alisema huyo kwenye kikao na hadi tunakwenda mitamboni hakupatikana.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق