Nahodha akosoa Muungano serikali tatu,mkataba

Waziri Kiongozi Mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha.
Waziri Kiongozi Mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha (pichani), amesema muundo wa  Muungano wa serikali tatu si muafaka na kama ungekubaliwa kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, utekelezaji wake ungekuwa mgumu.
Shamsi alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa  Ijitimai, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, jana.

Alisema Bunge Maalum la Katiba lilitafakari kwa kina mfumo wa Muungano wa mkataba na mfumo wa Muungano wa Serikali tatu na kuona utekelezaji wake kiuhalisia ni mgumu na kuamua kubaki katika Muungano wa serikali mbili kwa maslahi ya muungano wenyewe na wananchi wake.

Alisema wakati ya kujadili muundo wa  Muungano, waligundua kuwa ili kuingia wa mkataba ni lazima kwanza Muungano wenyewe uvunjwe na kama kama ingeshindikana kuafikiana ingekuwa ndiyo mwanzo wa kuvunjika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 50 na kuwafanya Watanzania kuishi kama ndugu.

Kuhusu muundo wa serikali tatu uliokuwa ukipendekezwa, alisema  haukuwa na tofauti na wa serikali mbili kwa kuzingatia Zanzibar isingeweza kupata kiti Umoja wa Mataifa, kuwa na sarafu yake, uraia, hati ya kusafiria, jeshi na Benki Kuu yake.

“Lazima wananchi mfahamu tulitafakari mfumo wa Muungano wa mkataba na ule wa serikali tatu tukaona utekelezaji utakuwa mgumu na muundo wa serikali tatu haukuwa na ubavu wa kuleta mamlaka kamili ya Zanzibar,” alisema Nahodha ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Alisema wapo Wazanzibari wanaamini  Zanzibar nje ya Muungano itakuwa tajiri, jambo ambalo siyo kweli kwa sababu visiwa hivyo kabla ya hapo vilitawaliwa na wakoloni kwa miaka 200 nyuma kutoka Oman na hadi Mapinduzi ya Mwaka 1964 ilikuwa nyuma kimaendeleo.

Aliwataka wananchi waisome kwa kina Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba ili utakapofika wakati wa kuipigia kura wafanye uamuzi sahihi wa kuikubali au kuikataa badala ya kupotoshwa na wanasiasa wasiotaka Muungano.

Alitaja mambo ambayo Zanzibar itanufaika nayo katika Katiba mpya inayopendekezwa kuwa ni, mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano na Zanzibar kuwa na mamlaka ya kujiunga na jumuiya za kikanda na nchi za visiwa ikiwamo OIC.

Mengine ni Zanzibar kuwa fursa ya kukopa nje, Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Pili Rais wa Muungano na kuanzishwa kwa tume ya kuratibu na kusimamia mgao wa mapato ya vyazo vya mapato vya Muungano.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم