Fundi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) akifanyia marekebisho moja ya mabasi ya shirika hilo.
Wakazi wa Dar es Salaam wataanza kupokea huduma zilizoboreshwa zaidi
kila watakapotumia mabasi yanayomilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es
Salaam (UDA), hii inatokana na mafunzo ya mwezi mmoja yanayotolewa na
shirika kwa madereva, makondakta pamoja na wafanyakazi wengine wa
shirika hilo.
Akizungumza wakati wa ziara fupi ya waandishi wa habari katika makao
makuu ya UDA jijini Dar es Salaam Jana, Mkuu wa kitengo cha mahusiano ya
umma wa UDA, Bw. George Maziku alisema kuwa miongoni mwa mambo
mengine, kampuni yake imejikita katika utoaji wa mafunzo madhubuti kwa
wafanyakazi wake ili kuboresha huduma zote zinazotolewa kwa wateja wa
UDA.
“Uongozi wa UDA unalichukulia kwa uzito mkubwa sana suala la usalama.
Tumeupitia mtaala wa utoaji elimu kwa wafanyakazi wetu lengo likiwa ni
kuboresha usalama na kufanya wateja wetu wafurahie hudumazinazotolewa na
shirika. Tunatoa mafunzo haya kwa madereva wetu ili kuinua hali yao ya
uzingatiaji wa usalama,” alisema Maziku.
Mbali na masuala ya usalama, mkuu huyo wa kitengo cha uhusiano
aliahidi uboreshaji wa huduma kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwajali
wateja, suala ambalo limekua likizua mjadala mkubwa.
Bw. Maziku alisema kuwa kampuni yake ina mabasi yapatayo 400 jambo
linayoifanya UDA kuwa kampuni ya kwanza Tanzania kuwa na magari mengi
yanayofanya kazi kwa mkupuo, hivyo kuna uhitaji mkubwa sana wa kuweka
viwango thabiti ambavyo vinaweza kuigwa na makampuni mengine.
“Tunalenga kuwa na mabasi 3000 ifikapo mwakani lakini kikubwa zaidi
kabla hata ya kupata idadi hiyo ya mabasi ni kuwapa mafunzo madereva
wetu ili wawe na elimu ya kutosha na uzoefu wa kutosha katika sekta ya
usafirishaji wa umma.
“Kwa kulitambua hili, kampuni imeajiri wakufunzi kutoka ndani na nje
ya nchi, ili kutoa mafunzo kwa madereva wetu na wafanyakazi wengine
wanaojihusisha na usafirishaji, mafundi na wafanyakazi wote (hasa
makondakta) katika kuwajali wateja,” alisema.
Bw. Maziku alisema kuwa mbali na mafunzo hayo, kampuni imekuwa
ikifuatilia kwa karibu sana tabia na mienendo ya madereva na makondakta
wake mara kwa mara kwa kuwatumia wasimamizi ambao hupanda mabasi ya
kampuni hiyo bila ya makondakta na madereva kupewa taarifa.
Kwa sasa, mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na kampuni hapo awali,
yameonyesha kuzaa matunda yaliyotarajiwa kwa kuwabadilisha baadhi ya
madereva na makondakta wa kampuni hiyo.
Hii ilibainika baada ya mkazi wa Dar es Salaam, ambaye amekuwa
akitumia huduma za UDA kwa nyakati tofauti, Bw. Andrew Sanga , kukiri
kuwa madereva wa UDA wapo tofauti ukilinganisha na madereva wengine wa
mabasi ya abiria.
إرسال تعليق