Kampeni ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya inayoitwa ‘Tuonane
Januari’ inazidi kupamba moto na wiki hii jumla ya wasanii 10 watapanda
jukwaa moja jijini Mwanza kwa kazi moja tu, kuwaambia vijana wenzao
kushiriki katika zoezi la kujiandikisha daftari la wapiga ili kuleta
mabadiliko katika uchaguzi wa mkuu ujao.
Kampeni hii imekuja baada ya kubainika kwamba
vijana wengi ni waongeaji wazuri wa kwenye majukwaa na kila kukicha
hulalamika kuhusiana na jinsi maendeleo ya nchi yanavyochelewa lakini
unapofika wakati wa kupiga kura hawajitokezi au wanashindwa kupiga kura
kutokana na kutokuwapo kwenye orodha.
Habari za ndani kutoka kwa wahusika wakuu wa
kampeni hiyo inayohamasisha vijana kujitokeza kupiga kura na kuchagua
viongozi vijana, bila kujali itikadi za vyama vyao, kufikia wiki ijayo
itakuwa inageuza mwelekeo kwa kuweka hadharani, nani na nani wataanza
kuungwa mkono na kundi hilo la wasanii kumi, watayarishaji wawili wa
muziki na wadau mbalimbali.
Dhana nzima imekuja kwa kutokana na nguvu ya
vijana, ambao wametajwa kuwa ndiyo nguzo ya mabadiliko iwapo wataamua
kubadilisha fikra zao na kushiriki kikamilifu kwenye hatua muhimu za
mabadiliko ya uongozi wa taifa lao, huku lengo kuu likiwa ni kuweka
viongozi wa kisasa wenye mwelekeo wa kitaifa zaidi na siyo wa kisiasa.
Kwa wiki ya tatu mfululizo sasa, hili limekuwa
somo linalotolewa kila kukicha, katika viwanja mbalimbali vya wazi,
ambako kampeni hizi zinaendeshwa, huko, muunganiko wa wasanii na
watayarishaji wa muziki hufanya mikutano inayoambatana na maonyesho ya
bure, ikiwa ni sehemu ya kwanza ya kampeni kubwa itakayohimiza vijana
kushiriki uchaguzi mkuu ujao ili kuweza kuchagua viongozi hasa vijana na
wale wenye mitazamo chanya kwa maendeleo ya Tanzania.
Akiongea mbele ya umati wa vijana wapatao 10,000
waliohudhuria onesho la pili kufanyika nchini, lililofanyika Jumanne ya
wiki hii viwanja vya sabasaba mjini Morogoro, Msanii Zuwena Mohamed
`Shilole’, amesema baada ya miaka 50 ya kutawaliwa kisiasa baada ya
Uhuru sasa ni wakati wa kuwa na uongozi wa kisasa ambao hautajali
kiongozi ametoka chama gani, ili mradi tu awe kijana au kiongozi mwenye
sifa za kuwa kiongozi bora, umoja huo umeahidi kuwaunga mkono watu wa
namna hii.
“Ni wakati sasa wa kuachana na siasa, kudanganywa
kila siku tumechoka, na kiukweli katika nchi hii vijana ndiyo wengi na
tuna nguvu, hivyo tukiamua kuibadilisha nchi kwa nia njema tunaweza”,
alisema Shilole.Kwa upande wake Nickson Simon, maarufu kwa jina la Nikki
wa Pili kutoka katika kundi la Weusi alisema siasa ni jinamizi
lililowagawa vijana kwa muda mrefu na kusababisha wakose umoja na kuwa
na kauli moja kwa masilahi ya nchi. Pia, wao kama wasanii wameligundua
hilo na wameamua kujitolea kutoa elimu kwa makundi ya vijana, na
kuliweka pembeni na kuangalia mustakabali wa nchi.
“Kilichopo hapa vijana wenzangu ni kupiga chini
siasa na kukubali usasa, tuangalie viongozi vijana wenye akili, tuachane
na hivi vyama vinatupoteza,” alisisitiza Nikki.
Kampeni za Tuo8 Januari, zilianza wiki mbili
zilizopita na zilizinduliwa Idara ya Habari Maelezo, huku msanii Fareed
Kubanda akiwa kiongozi wa kampeni hiyo na tamasha la kwanza lilifanyika
Jumapili ya tarehe 14, Desemba mwaka huu, katika Viwanja vya Sabasaba,
mjini Njombe. Kwa mujibu wa Kubanda, kampeni hizi zinatarajiwa kuzunguka
nchi nzima na kuanzia mwezi wa kwanza, muunganiko huo huenda ukaanza
kutaja viongozi ambao wataanza kuwaunga mkono katika kampeni zao.
Mpaka sasa kampeni hiyo inajumuisha jumla ya
wasanii 10 ambao wameamua kuzunguka nchi nzima kuhamasisha vijana wenzao
kuleta mabadiliko ambao ni MwanaFA, Ditto, Fid Q, Nikki wa Pili,
Shilole, Mwasiti, Linah, Godzilla, G Nako na Stamina.Wadau wengine
wanaoshiri.ki kampeni hizi kwa kujitolea ni Watayarishaji P Funk na
Lamar, pamoja na wadau Said Fela na Babu Tale.
Harakati ya Tuo8 Januari hazijafunga milango na wasanii wengine wataendelea kujiunga katika kampeni hizi.
Wiki ijayo wanatazamia kuwa Mwanza siku ya Jumapili tarehe 28-Desemba-2014.
- Mwananchi
- Mwananchi

إرسال تعليق