Tanzania ina kila aina ya vituko. Muuza nguo anakuletea shati,
badala ya kutaja bei anakuuliza “unataka kununua shilingi ngapi?” Una
dhahabu mkononi, unapotaka kuiuza mnunuzi haangalii ina ubora au daraja
gani. Anakuuliza “dhahabu hii imefanana na ya nani?” Kama inafanana na
ile ya Juma utalipwa kama alivyolipwa Juma. Kama imefanana na aliyouza
Mr. Smith basi nawe utalipwa kama alivyolipwa Mr. Smith.
Ukitaka kununua tai mtaa wa Samora, utauziwa kwa
bei ya mtaa huo. Lakini kama utabahatika kukutana na mchuuzi huyo mtaa
wa Kongo, basi tai hiyo itauzwa kwa bei ya mtaa wa Kongo. Unapoenda
kuomba tenda ya kulisha kampuni unaangaliwa ubora wa kitambi chako na
siyo elimu au uzoefu wako katika ugavi.
Hili linawakuta sana vijana wanaochipukia kwenye
sanaa. Anapoenda kwa mfadhili kwa mara ya kwanza inaangaliwa sauti yake
imefanana na ya nani na hata sura yake imefanana na mwimbaji gani. Kama
hana hali ya kufanana na nguli, ni lazima awe bingwa wa kupesti ndipo
afadhiliwe.
Kabla sijalielewa hili vizuri, nilifikiri huo ni
mfumo wa dunia nzima. Niliitazama Marekani na marais wake, nikaona wapo
waliofanana kupita maelezo. Hata wewe nikikueleza jinsi Abraham Lincoln
na JFK (John F, Kennedy) walivyooana (sorry, walivyofanana) huwezi
kuniamini. Lakini ndiyo ukweli kamili; Ebu tazama:
Abraham Lincoln alichaguliwa Congress mwaka 1846
wakati John F. Kennedy alichaguliwa Congress mwaka 1946. Lincoln
akachaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1860 na Kennedy akachaguliwa
kuwa Rais wa Taifa hilo mwaka 1960. Wote walijihusisha zaidi na haki za
binadamu wakati wa uongozi wao.
Wake zao wote wawili walipoteza watoto wakiwa
Ikulu ya Marekani. Kila mmoja wa marais hawa alipigwa risasi ya kichwa
Ijumaa. Msaidizi wa Rais Lincoln aliitwa Kennedy na wa Rais Kennedy
aliitwa Lincoln. Mrithi wa Lincoln aliitwa Johnson, kadhalika wa Kennedy
aliitwa Johnson.
Johnson wa Lincoln alizaliwa mwaka 1808, na wa
Kennedy alizaliwa mwaka 1908. Muuaji wa Lincoln alizaliwa mwaka 1839 na
wa Kennedy alizaliwa mwaka 1939. Wauaji hawa walijulikana kwa majina yao
matatu matatu yenye herufi kumi na tano.
Lincoln alipigwa risasi kwenye jumba la sinema
lililoitwa Ford na muuaji akakimbilia kujificha kwenye ghala. Muuaji wa
Kennedy alipiga risasi kutoka ghalani na kujificha kwenye jumba la
sinema lililoitwa Lincoln na lililojengwa na Ford. Tena basi wauaji wao
nao waliuawa kabla ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Unaona kufanana huko? Basi nikajua Kennedy
alisafiria nyota ya Lincoln. Lakini kichwa kiliniuma sana kwa kujiuliza:
kama sote tungefanana, ni nani angemwongoza mwenzake? Au kumwimbia
mwenzake? Ni wazi kuwa binadamu wote ni sawa, lakini hata kama unaandika
kama Shaaban Robert, utakuwa na mashairi yake?
Ni wazi pia kwamba kila mtu ana akipendacho
tofauti na wengine. Kama wewe unapenda nyimbo za hip-hop, kuna
wanaopenda nyimbo laini. Hao wanaopenda nyimbo laini pia wana vituko
vyao. Huyu anapenda sauti nyororo kama za akina Dolly Paton, yule
anataka sauti nzito zenye mikwaruzo kama ya Barry White. Kumbe ndiyo
maana vipaji tofauti vinapaswa kuheshimiwa. “Half of the story has never
been told” (nusu ya hadithi bado haijatolewa hadharani). Kila kipaji
kipya kinapoibuka kinakuja na asilimia sufuri nukta sufuri sufuri kama
mia, mwisho moja ya jambo jipya.
Pengine tofauti na wenzetu, wasanii wetu wachanga
wanalazimika kuvaa kama fulani, kutembea kama fulani na kuigiza kama
fulani ili wafanikiwe. Pia ndiyo maana sanaa yetu inaporomoka kadiri ya
muda unavyokwenda. Hakuna kipya. Laiti tungelijua dada Halle Berry
(mwigizaji mshindi wa Tuzo za Oscar na Emmy) alihamia New York akiwa
hana pa kulala pale. Alikesha na yatima na baadaye akahamia kwenye
makazi ya wasio na makazi yaliyomilikiwa na kituo cha YMCA. Wadau
walimuibulia hapo.
Hakuna mtu asiyemjua Charlie Chaplin (usipomjua
kwa jina hilo utamjua kwa “Chale Mwembamba”). Huyu naye ni mshindi wa
tuzo za Oscar kwa uandishi, uigizaji, uongozaji na uzalishaji wa sanaa.
Alikuwa mzururaji jijini London baada ya baba yake kufa na mama yake
kupata uchizi. Lakini baada ya kugunduliwa kipaji chake cha kipekee,
aliifundisha dunia kuwa komedi nazo ni mali.
- Mwananchi
- Mwananchi

إرسال تعليق