Jana katika tovuti hii tulitoa habari iliyowakariri viongozi wa
dini wakionyesha kukerwa na vitendo vya ufisadi, wizi, uzembe ikiwamo
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Viongozi hao waliokuwa wakitoa mahubiri yao katika
ibada ya Sikukuu ya Krismasi walisema ugumu wa maisha, ukosefu wa
ajira, kukosa uhakika wa huduma bora za matibabu na elimu ni moja ya
matatizo makubwa ambayo hivi sasa yanalisumbua taifa.
Walisema mbali na maisha ya ufukara na ukosefu wa
huduma, sakata la escrow na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliyotolewa
Jumatatu vimezidi kuzidisha hofu kwa Watanzania na kuwafanya waonekane
kama hawana matumaini.
Walisema watu wengi wanaishi katika ulimwengu wa
hofu kutokana na ufukara, ukosefu wa huduma, na kwamba watu wanajiuliza
watawasomeshaje watoto wao na watapata wapi huduma bora za matibabu.
Walienda mbali zaidi ya kueleza kuwa fedha
zilizochotwa katika akaunti ya escrow ni mali ya umma, kutokana na
taarifa iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC).
Kwa ujumla ni kwamba ujumbe wa viongozi wa dini ulikuwa unatoa somo kwa Serikali kwamba sasa inapaswa kuzuia matendo haya maovu.
Pia, ujumbe huo ulikuwa unawakumbusha viongozi wa Serikali wajibu wao wa kuwapatia maisha bora wananchi.
Wananchi wanashangaa kuona wakati wao wanaishi
katika maisha magumu, lakini baadhi ya viongozi wakionekana wakihusishwa
kuchota mamilioni ya fedha za umma bila ya kuchukuliwa hatua stahiki.
Zipo kashfa nyingi ambazo zimetokea hapa nchini
mpaka sasa, lakini kwa sababu hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na
zingine zinaendelea kuibuka kila siku.
Katika utawala wa awamu ya nne ambao ndiyo
unaonekana kukumbwa na kashfa nyingi zaidi, ilianza na Kashfa ya
Richmond, kashfa ya wizi Katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa),
Operesheni Tokomeza na sasa escrow.
Pamoja na kwamba kashfa hizi ziliitikisa Serikali
kwa kila moja kwa wakati wake, kwa Richmond aliyekuwa waziri mkuu Edward
Lowassa na mawaziri wengine walilazimika kujiuzulu na kashfa ya Epa
walioiba walipewa muda wa kuzirejesha na kwa walioshindwa walifikishwa
mahakamani.
Kashfa ya Operesheni Tokomeza iliwang’oa mawaziri
wanne na kashfa ya escrow tayari imewang’oa vigogo wawili, mmoja
kasimamishwa kazi na mwingine kawekwa kiporo.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment