Rais Jakaya Kikwete
Azimio linalomweka kwenye mtihani mkubwa Rais Kikwete ni kuwafuta kazi Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, kwa kuhusika na kashfa hiyo.
Mtihani huu mkubwa na mgumu unaangukia mikononi mwa Rais Kikwete baada ya juhudi za baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawaziri wiki iliyopita kujaribu kwa mbinu mbalimbali kutokutolewa azimio ambalo lingeelekeza moja kwa moja hatua za kuchukuliwa dhidi ya viongozi waandamizi wa serikali waliohusika katika kashfa hiyo kukwama.
Mbali na Muhongo na Maswi, pia Rais Kikwete atatakiwa kumfuta kazi Mwansheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, anayetajwa kama mtumishi wa umma aliyeandika nyaraka mbalimbali kusukuma maamuzi ya kuondolewa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zaidi ya Sh. bilioni 300 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Ingawa hadi Ijumaa usiku wa saa nne, wahafidhina wanaotaka kulindana ndani ya CCM na hata baadhi ya mawaziri walikuwa wamefanikiwa kupunguza makali ya maazimio ya Bunge yaliyokuwa yamependekezwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ilipewa jukumu ya kupitia ripoti za uchunguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kibao kiligeuka wakati wa azimio kuhusu adhabu inayostahili Prof. Muhongo.
Mtihani huu mkubwa wa Rais unamgusa sana kwani hii itakuwa ni mara ya nne anateua Waziri wa Nishati na Madini tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Mawaziri walioshikilia nafasi ya wizara hiyo na kuondolewa ni pamoja na Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, William Ngeleja na sasa Pro. Muhongo. Kila mmoja katika waliokalia kiti hicho walikumbana na sakata mojawapo, lakini ambalo limethibitika kuchotwa kwa mabilioni ya fedha za umma ni Tegeta Escrow.
Ingawa madaraka ya uteuzi wa vigogo hao ni ya Rais Kikwete, kwa jinsi hali ilivyo, itakuwa ni vigumu kupuuza kuwafuta kazi Prof. Muhongo na Maswi kwa sababu kufanya hivyo atakuwa ameingia kwenye mgogoro wa moja kwa moja na Bunge linalotawaliwa kwa asilimia kubwa na chama chake.
Hali hiyo ikitokea, serikali itakuwa imeamua kukumbana na mapambano na wabunge wake wakisidiana na wale wa upinzani, hali ambayo inaweza kudhoofisha serikali kwa kiwango kikubwa.
Ingawa Rais Kikwete anaelekea ukingoni mwa utawala wake, bado ana mambo makubwa matatu ambayo yatahtaji maamuzi ya Bunge la sasa, mosi; bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/16 itahitaji baraka za Bunge; mabadiliko ya sheria ya uchaguzi hasa kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi yanahitaji baraka za Bunge; lakini pia utungwaji wa sheria mbalimbali kati ya sasa na Juni kabla ya Bunge kuvunjwa zitahitaji baraka za Bunge pia.
Ukiweka mbali shinikizo la Bunge, Rais Kikwete akiwa ndiye Mwenyekiti wa CCM, anakabiliwa na changamoto kutoka makundi na makada wa aina mbalimbali wa chama hicho, juu ya usafi wa baadhi ya vingozi waandamizi serikalini.
Sakata la Tegeta Escrow linafananishwa kwa karibu sana na lile la Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya BoT, ambako takribani Sh. bilioni 133 zilichotwa kifisadi.
Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana na timu yake ya sekretariati, kwa nyakati tofauti kwenye ziara zao mikoani, wamekuwa walirusha mashambulizi dhidi ya baadhi ya mawaziri ambao ama wamewaita mizigo kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao sawa sawa, au wale ambao wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kiasi cha kuwafanya wananchi waichukie serikali na chama tawala.
MAAZIMIO HAYA HAPA
Katika kikao juzi, Bunge lilitoa maazimio manane, likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema kwa kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 321 kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa BoT.
Wengine waliopendekezwa kuvuliwa yadhifa zao ni wanakamati wa kamati za kudumu za bunge hilo, William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa.
Pia wamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisoma maazimio hayo baada ya kufikiwa kwa maridhiano baina ya kamati hiyo, kambi ya upinzani bungeni na Chama Cha Mapinduzi.
Zitto alitaja maazimio hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini wanapaswa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).
Bunge pia lilitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na wale watakaobainika kuhusika kwenye vitendo hivyo vya jinai.
Bunge pia lilitaka Kamati za Kudumu za Bunge kuwavua nyadhifa wanakamati wake wakiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, Chenge na Ngeleja wametajwa kunufaika na fedha za mwanahisa Rugemalira kwa Chenge kupewa Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. milioni 40.2.
Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa kwenye kashfa hiyo.
Majaji waliotakiwa na Bunge kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ni pamoja na Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Bunge pia lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق