Arusha/Zanzibar. Siri ya kunusurika kwa Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow imebainika
kuwa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano walikubaliana kumwacha kutokana na
kubakiza muda mfupi na pia kukwepa kuvunja Baraza la Mawaziri kwa mara
ya pili.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo walioandaa
maazimio manane ya Bunge, Dk Hamis Kigwangalla alisema jana kuwa bila
kufikia makubaliano ya kumwacha Pinda, mwafaka usingepatikana baada ya
kuwapo makundi mawili yenye kukinzana kuhusu pendekezo la kutaka Pinda
awajibike.
“Kama ulivyoona bungeni, wabunge wengi wa CCM,
walikuwa wakimtetea Waziri Mkuu, wakitaka asing’oke kutokana na
mapendekezo ya PAC, hivyo tukaona ili kufikia maridhiano ni bora
kuwaondoa mawaziri na watendaji ambao wameguswa moja kwa moja katika
kashfa hii na kumwacha Waziri Mkuu ambaye hakuhusika moja kwa moja,”
alisema.
Hata hivyo, alisema kufikia maridhiano hayo,
haikuwa kazi rahisi kwani wabunge wa upinzani walitaka mawaziri
watimuliwe na Pinda awajibike kwa kuwa ndiye mtendaji Mkuu wa Serikali.
“Kimsingi hakuna sehemu hata moja ambayo Waziri
Mkuu ameonekana kuhusika moja kwa moja na sakata hili, ndiyo sababu
iliyomfanya abaki salama,” alisema.
Dk Kingwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Tamisemi, alisema Bunge lingefanya makosa kama lingeshindwa
kuwawajibisha mawaziri hao.
Zanzibar walia na Pinda
Wanasiasa na wanaharakati wa Zanzibar wameelezea
kushangazwa na kitendo cha Bunge kumwacha Pinda wakidai kuwa alitakiwa
awajibike.
Mwanasiasa mkongwe, Soud Muhanna Nassor (74)
alisema kama waziri mkuu Serikali ipo chini yake, alitakiwa kujiuzulu
ili kurejesha imani kwa wananchi.
Aliyekuwa mgombea urais wa Muungano kwa tiketi ya
TLP 2010, Abdallah Othman Mgaza (70) alisema kimsingi uamuzi uliofanywa
na Bunge umezingatia zaidi utashi wa kisiasa badala ya kusimamia kanuni
na sheria.
Rashid Salum Adiy (52) alisema licha ya uamuzi uliofanywa na Bunge kutia moyo, Pinda naye alitakiwa ajiuzulu wadhifa wake.
pamoja na mawaziri na watendaji ambao wamehusishwa
ili kuendeleza misingi ya uwajibikaji wa pamoja kama alivyowahi kufanya
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق