Dar es Salaam. Wajumbe wa kamati tatu za Kudumu za Bunge ambazo
wenyeviti wake wanatakiwa kuvuliwa nyadhifa zao kutokana na kuhusika
katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, ‘wanasuasua’ kuwaondoa na
kuchagua viongozi wengine.
Kwa nyakati tofauti wajumbe wa kamati hizo ambazo
ni Bajeti, Nishati na Madini na Katiba, Sheria na Utawala wamekuwa
wakishangazwa na hatua za wahusika hao kuendelea kujitambulisha kuwa ni
wenyeviti, sambamba na kuongoza vikao vya kamati hizo, wakati wakijua
wazi kuwa hawatakiwi kufanya hivyo.
Wenyeviti wanaotakiwa kuachia nyadhifa zao ni
Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba) na
Andrew Chenge (Bajeti).
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah aliliambia
gazeti hili jana kwamba jukumu la kuwaondoa wenyeviti hao lipo mikononi
mwa wajumbe wa kamati hizo, kwamba kama wakishindwa Spika wa Bunge
atachukua jukumu hilo.
Katika mkutano wake wa 16 na 17, Bunge liliazimia
kuwa watu walioshiriki katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow
wakiwepo viongozi wa Kamati hizo tatu, wachukuliwe hatua za haraka na
Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge
unaotarajiwa kuanza Januari 27 mwaka huu.
Akinukuu azimio hilo Kashilillah alisema, “Wajumbe
husika ndiyo wanaotakiwa kuwaondoa wenyeviti hao, hilo ni lazima
mlitambue jamani. Waulizeni ni lini watafanya hivyo.”
Alisema ndiyo maana kamati ikiwa haina mwenyekiti,
wajumbe wenyewe huchagua mmoja kati yao kwa ajili ya kuongoza kikao cha
kamati.
“Spika hawezi kumwondoa mwenyekiti wa kamati
husika, anachoweza kufanya Spika ni kumhamisha mwenyekiti kutoka kamati
moja kwenda nyingine. Akifanya hivyo maana yake ni kwamba mwenyekiti
husika anapoteza sifa za kuwa mwenyekiti,” alisema.
Alisema jambo hilo Spika Makinda anaweza kulifanya
kama wajumbe wa kamati hizo tatu zitashindwa kuchagua wenyeviti
wengine. Kuhusu Chenge ambaye aliteuliwa na Spika Makinda kuwa
mwenyekiti wa kamati ya Bajeti alisema, “Chenge aliteuliwa katika
kipindi cha mpito ambacho kikiisha atachaguliwa mwenyekiti mwingine.
Hivyo naye anaweza kuondolewa tu na wajumbe wa kamati.”
Mvutano katika kamati
Taarifa kutoka ndani ya kamati ya Bajeti zilieleza
gazeti hili kwamba, juzi kamati hiyo ilikutana na Wizara ya Maji na
Uchukuzi na Chenge alijitambulisha kama mwenyekiti, jambo ambalo
liliwashangaza wajumbe wa kamati hiyo.
“Tumeshangazwa jinsi alivyojitambulisha kwa sababu
awali kamati tulikubaliana kuwa akae pembeni na kumwachia Makamu
mwenyekiti, Dk Limbu (Festus) kuongoza vikao vya kamati. Inavyoonekana
ni kama anang’ang’ania nafasi hii,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati
hiyo.
Post a Comment