Dar es Salaam. Wakati Halmashauri Kuu ya Chama
cha ACT-Tanzania ikikutana kujadili agenda tatu, ikiwamo ya kuazimia
kumvua uongozi Mwenyekiti, Kadawi Limbu, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa leo inawakutanisha viongozi waandamizi wa chama hicho kusaka
suluhu ya mgogoro wao.
Chama hicho kwa siku za hivi karibuni kimekuwa
katika mvutano kati ya Limbu na viongozi wenzake, hasa Katibu Mkuu,
Samson Mwigamba.
Viongozi wengine wanaosubiriwa na rungu la kikao
cha halmashauri kuu ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), Leopold Mahona na
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Grayson Nyakarungu.
Juzi gazeti hili lilimnukuu, Msaidizi wa Msajili
wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza akisema: “Mvutano huu hata sisi
tunausikia, tumeamua kuwaita Jumanne hii (leo) ili tuwasikilize wote kwa
pamoja.”
“Tumewaita siyo kwa lengo la kuendeleza tofauti zao, bali kuzimaliza baada ya kusikiliza kila upande.”
Akifungua kikao cha halmashauri kuu jana, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Tanzania (Bara), Shaban Mambo alisema:
“Mkutano huu ni halali kisheria, kikatiba na
kikanuni, hivyo nawasihi wajumbe msiwe na hofu na mjadili kwa kujenga
hoja na unapokuwa huelewi usiogope kuuliza.”
Aliongeza: “Kila chama lazima kipite katika
matatizo na unapopita katika matatizo kama haya ndiyo chanzo cha
mafanikio na kukua kwa demokrasia, hatutaogopa kusema ukweli na kutenda
haki ni jadi yetu.”
Akitaja ajenda za kikao hicho, Mwigamba alisema ni
kupokea na kujadili taarifa ya chama kuhusu Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Akifafanua ajenda hizo alisema, watapitisha
mapendekezo ya ratiba ya uchaguzi wa ndani iliyopendekezwa na Kamati Kuu
Januari 5, mwaka huu kuanzia Januari 19 hadi Machi 28 mwaka huu.
Aidha, watajadili taarifa ya hali ya kisiasa ndani
ya chama, ikiwamo taarifa ya kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza
tuhuma dhidi ya Limbu na wenzake.
Kuhusu akidi alisema kikao hicho kinapaswa kuwa na
wajumbe 88 na akidi yake ni asilimia 50, ambayo ni sawa na wajumbe 44
na waliohudhuria walikuwa wajumbe 63 ambao wamevuka idadi inayotakiwa.

إرسال تعليق