Sakata la jengo la ATCL kupigwa mnada laibuka tena

Dar es Salaam. Kampuni tatu zimewasilisha maombi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara zikitaka jengo la Makao Makuu ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lenye thamani ya Sh12 bilioni lipigwe mnada kufidia madeni yao yanayofikia zaidi ya Sh2 bilioni.
Wadai hao ni Kampuni ya Huduma za Utalii ya Leisure Tours and Holidays, inayodai Dola 477,506.38 za Marekani, Kampuni ya Huduma za Hoteli ya Wellworth Hotels & Lodges Ltd inayodai Dola 661,089 na Kampuni ya Huduma za Pembejeo ya Tanzania Bags Corporation 1998 (TBC), inayodai Dola 44,000.
Septemba 2014, kampuni hizo kwa nyakati tofauti ziliingia makubaliano na Wizara ya Uchukuzi na ATCL ya ulipwaji wa madeni hayo.
Serikali na ATCL waliahidi kulipa madeni hayo kwa awamu tatu, kuanzia Oktoba hadi Desemba 2014, lakini hadi sasa mdaiwa hajalipa.
Wadai kupitia kwa wakili wao, Msemwa & Company Advocates, wameiandikia barua mahakama hiyo wakiomba iendelee na utekelezaji huo.
Katika barua hiyo ya Januari 8, 2015 iliyosainiwa na Wakili Jerome Msemwa, kwenda kwa msajili wa mahakama hiyo, wadai hao wanaiomba Mahakama iamuru jengo hilo lililoko katika Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam liuzwe.
“Kwa unyeyekevu tunaomba dalali wa mahakama ateuliwe ili kuuza jengo hilo, kufidia deni linalodaiwa, bila kuchelewa,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Wellworth ililifungulia ATCL kesi ya madai namba 56 ya mwaka 2010 kutokana na gharama za huduma za malazi kwa maofisa wa ATCL, huku deni la Leisure likitokana na gharama za ukodishaji magari.

Post a Comment

أحدث أقدم