Mrema akinyoshea vidole Ukawa akikituhumu kwa kuhujuma

Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, Agustino Mrema.
Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, Agustino Mrema, amesema amebaini njama za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukihujumu chama chake, ili kishindwe uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kadhalika amewatumia salamu  wale wanaoleta ‘chokochoko’ dhidi yake akisema  TLP ni ngangari  na hakuna wakuing’oa.

Mrema alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na wanahabari kuzungumzia njama za upinzani kumtishia kisiasa, akitaja kikundi cha waasi  30  kinachoongozwa na Joram Kinanda aliyejipachika cheo cha Mwenyekiti Taifa.

Alisema Kinanda kupitia kundi hilo amekuwa akiibuka wakati wa uchaguzi wa TLP, kwa lengo la kuuvuruka.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, Mrema alisema licha ya NCCR-Mageuzi na Chadema kumvamia jimboni kwake kwa mbwembe za kuchukua viti vingi katika uchaguzi huo, waliburuzwa na CCM iliyojipatia ushindi wa kishindo cha sunami.

“Mbatia alipata kura 17 na Chadema kura 15 na TLP tulipata kura nane baada ya wagombea wangu kurubuniwa kwa  Shilingi 2,000,000,” alisema.
Alisema hila hizo zinalengo la kumfanya Mrema asipate ubunge pamoja na kumtoa kwenye nafasi ya uenyekiti.

Mrema alisema kampeni hiyo chafu dhidi ya TLP ndiyo iliyomfanya Katibu Mkuu wa chama hicho, Jeremiah Sherukindo kuondoka ndani ya chama kwa maneno machafu.

“Wakati Sherukindo akiwa TLP, mke wake alikuwa Kirua Vunjo kupitia chama cha  NCCR-Mageuzi akikisaidia, hamuoni huu ni mchezo mchafu wa Ukawa dhidi ya Mrema, yanayotokea leo na kikundi hichi kinachotokea kipindi cha uchaguzi nakiambia hivi, TLP haitikisiki,” alisema.

Kuhusu kikundi hicho ambacho mwenyekiti huyo alisema kimerusha shutuma mbalimbali dhidi yake pamoja na chama na kudai, kuwa yeye sio Mwenyekiti halali kutokana na muda wake kuisha,  Mrema alikijibu kuwa, kwa mujibu wa katiba ya chama cha TLP, uwenyekiti wake ni halali.

Pia alikijibu kikundi hicho kuwa, msajili wa vyama vya siasa, hatoi madaraka katika hilo bali hushauri kwa mujibu wa katiba ya chama na ndivyo alivyofanya baada ya kupokea sababu za kutofanyika uchaguzi huo.

“Chama kilikuwa hakina fedha na TLP inapokea Shilingi milioni 4.3 kila mwezi kama ruzuku, hivyo ili kuitisha mkutano mkuu unaotakiwa kuwa na zaidi ya wajumbe 160 tunahitaji zaidi ya milioni 30,” alisema.

Alisema kutokana na chama kukosa fedha za kuitisha mkutano mkuu kwa ajili ya uchaguzi, waliitisha kikao Aprili 3, mwaka jana ambapo walikubaliana kuyakasimu madaraka ya Halmashauri Kuu kwa Kamati kuu.

“Baada ya  hapo nilikwenda India kwa matibabu na huku nyuma uchaguzi wa Serikali za mitaa uliendelea ambao unahitaji fedha, tulimwandikia barua Msajili wa vyama kuhusu kuhairisha mkutano mkuu na alituelewa na alitujibu endapo hautafanyika kwa tarehe hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema.

Aidha alisema Kamati Kuu ilikuwa ikutane juzi lakini Naibu Katibu Mkuu Sera, Richard Lyimo, alipata msiba na ilikutana jana.

Lyimo aliwataka waandishi kumtafuta  Kinanda ili awaonyeshe tawi lake la chama lilipo kwa sababu ili mtu uwe mwanachama wa chama chochote cha siasa lazima utambuliwe huko.

Katibu huyo aliifananisha TLP na mti unaopenda ambao hupigwa mawe na kusisitiza kuwa, chama chake kimejipanga kushika dola.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم