Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia.
Hatua hiyo ya Nec inadaiwa kuchukuliwa kinyume cha makubaliano
yaliyofikiwa kati yake na wadau wakuu wa uchaguzi, ambao ni vyama vya
siasa.
Kutokana na hatua hiyo ya Nec, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu,
aliitisha kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge jana asubuhi ili kujadili
suala hilo kabla ya Bunge kuishauri serikali nini kifanyike.
Uamuzi huo wa Zungu ulitokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa
Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, bungeni jana, ambaye alitaka
Bunge lisimamishe shughuli zake za jana asubuhi ili kujadili suala hilo
aliloliita kuwa ni la ‘dharura.’
Mbatia alisema Nec juzi ilikutana na kuamua kuanza kundesha zoezi
hilo katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe bila wadau wakuu
kushirikishwa kama walivyokubaliana kwenye meza ya mazungumzo.
Alisema makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha wadau wakuu
kilichofanyika Januari 8, mwaka huu, kupitia Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) chini ya Mwenyekiti wake, John Cheyo, ambacho Nec
walialikwa.
Mbatia alisema katika kikao hicho, Nec iliwahakikishia kuwa zoezi
hilo lina changamoto kubwa na kwamba, lingeanza upya Januari 15, mwaka
huu.
Alisema zoezi hilo lilianza mwanzoni mwa Juni, mwaka jana, lakini
halikufanikiwa, pia likafanyika tena mwishoni mwa mwezi huo, katika
maeneo ya mkoa wa Rukwa, vilevile likafeli. Alisema wakakubaliana kuwa
Nec na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) wakutane na kujadili kwa
pamoja kisha wawaelimishe wadau namna zoezi hilo litakavyofanyika kwa
kutumia BVR ili wakubaliane kama lina maslani kwa taifa au la.
Mbatia alisema walifikia makubaliano hayo kwa kuwa iwapo jambo hilo halitaendeshwa vizuri nchi inaweza kuingia kwenye machafuko.
Hata hivyo, alisema juzi Nec ilikutana na kuanza kufanya utaratibu
wa kuendesha zoezi hilo katika mikoa hiyo bila wadau wakuu kushirikishwa
kama walivyokubaliana kwenye meza ya mazungumzo.
Alisema katika kikao hicho, walikubaliana kuwa zoezi hilo
lihakikishe linafanyika kwa uadilifu, uaminifu na kwa pande zote
kushirikishwa.
Mbatia alisema wadau waliokutana katika kikao hicho, wanatoka vyama
vyote vya siasa, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho
kiliwakilishwa na Makamu wake Tanzania Bara, Philip Mangula.
Alivitaja vyama vingine vilivyoshiriki kikao hicho cha wadau kuwa
ni pamoja na Chadema, iliyowakiloshwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod
Slaa, CUF (Prof. Ibrahim Lipumba), NCCR-Mageuzi (James Mbatia), TLP
(katibu mkuu wake) na vyama vingine visivyokuwa na uwakilishi bungeni.
Alisema jambo hilo lina maslahi mapana kwa umma na kwamba, katika kikao hicho, Nec ilieleza mambo mengi sana.
"Tukawashauri kwa nia njema kwamba, ni bora tukae, tuzibe ufa kabla ya kujenga ukuta tuaminiane," alisema Mbatia.
Alisema pia waliisisitiza kuwa Nec ulazima wa kulifanya jambo hilo
ili kuhakikisha kwenye uchaguzi mkuu malalamiko yanapungua na
kuhakikisha yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa Kenya, Ghana, Msumbiji
na Malawi yasitokee nchini.
Kutokana na hali hiyo, alisema kwa mujibu wa kanuni ya 47, Bunge
linapaswa kutekeleza matakwa ya ibara ya 63 (2) ya katiba ya nchi
inayotambua kazi ya Bunge kuwa ndiyo chombo kikuu cha kuisimamia na
kuishauri serikali ili zoezi hilo lifanyike kwa uadilifu na kwa ufanisi
mkubwa kuepuka mtatizo yaliyotokea katika nchi hizo yasitokee hapa
nchini.
"Na hakuna jambo jema kama kuaminiana katika jambo lenye maslahi kwa taifa," alisema Mbatia.
Akijibu hoja hiyo, Zungu alisema anakubaliana kwamba, jambo hilo ni
la muhimu, kukaa pamoja na Bunge kuwa ni chombo cha kuishauri serikali.
Hivyo, akaiagiza serikali kuanzia wakati huo kukaa pamoja na Mbatia wakalijadili kwenye Kamati ya Bunge ya Uongozi.
Hata hivyo, Kamati ya Uongozi, imelipeleka suala hilo kwenye Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili likafanyiwe kazi.
Katika kikao hicho, serikali imesisitiza kuwa imeshatoa fedha za kutosha kwa ajili ya BVR.
CHANZO:
NIPASHE

إرسال تعليق