KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA YA ROMBO YAKAA KWA DHARURA. CHADEMA WAALIKWA KWA MARA YA KWANZA KATIKA HISTORIA.
Juzi siku ya Jumanne tarehe 10/02/2015,kamati ya ulinzi na usalama Rombo ilikutana kwa dharura ili kujadili hali ya kiusalama Wilaya ya Rombo.

Kwa mara ya kwanza CHADEMA tulialikwa kwenye kikao cha kamati hiyo ili kutoa mchango wetu kuhusu namna ya kuifanya Rombo iwe na amani. Nilialikwa mimi kama Mkt wa CHADEMA(W) na pia Mbunge wetu Selasin alialikwa.

Lengo kubwa la kikao lilikuwa ni kujadili namna ya kurejesha utulivu Rombo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro bwana Leonidas Gama kuchafua hali ya hewa baada ya kikao chake na wenyeviti Wa vijiji na vitongoji kilichofanyika tarehe 5/2/2015 katika ukumbi wa shule ya sekondari Shauritanga. ambapo alidai kuwa zaidi ya ofisi 36 za vijiji katika Wilaya ya Rombo ni mali ya CCM.

Baada ya kauli ile pamoja na ubabe na vitisho vingi kwenye kikao ndipo viongozi Wa vijiji na vitongoji watokanao na CHADEMA walikasirika na kutoka nje na baadae huko vijijini ndipo ofisi zikaanza kuchomwa moto.

Baada ya Mkuu wa Wilaya kuona hali inaelekea kuwa mbaya,ilibidi asitishe kuhudhuria mapokezi ya Raisi mjini Moshi aliyekuwa anakuja kuzindua jengo kibiashara la NSSF ili abaki Rombo kushughulikia hali ya usalama.

Kwenye kikao tulikubaliana iundwe tume ya kuchunguza na kubaini ni nani mmiliki halali wa zaidi ya ofisi 36 za vijiji wilaya Rombo ambazo wananchi wanadai ni mali yao na pia CCM wanadai pia ni mali yao.

Tulikubaliana kuwa tume hiyo iwe na wajumbe kutoka halmashauri ya wilaya, CCM na pia CHADEMA ili kupunguza upendeleo.

Lakini pia tulikubaliana kuwa tume hiyo ipewe siku 60 za kukamilisha kazi yake na hadidu za rejea zitakazoiongoza namna ya kufanya kazi lakini pia hadidu hizo zitaweka mipaka ya uhuru wa time.


Pia tulikubaliana kuwa kwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo alishawaagiza watendaji Wa vijiji kuhama kwenye hizo ofisi,agizo hilo lisitishwe mara moja na waendelee kutumia ofisi hizo mpaka pale taarifa ya tume itakapotoka na kubainisha ukweli.

Pia tulikubaliana kuwa kwa zile ofisi ambazo hazikuwa na bendera za CCM kabla ya mgogoro huu lakini zikapandishwa baada ya mgogoro huu,basi zishushwe zote ili kuwaondolea wananchi taharuki kwamba CCM wamepora ofisi zao na wamepandisha mpaka bendera.

Lakini cha kushangaza katika kikao kile wenzetu wa CCM hawakualikwa. Nilipomuuliza DC juu ya sababu za kutowaalika CCM ilihali wao ni sehemu ya pande zilizohusika katika kusababisha migogoro hii, mkuu wa Wilaya alidai kuwa mimi yaani Mkt wa CHADEMA(W) ndiye niliyemshauri kuwa tukae kwa pamoja ili tuweke hali sawa na hivyo hakuona haja ya kuwaalika CCM.

Pamoja na majibu ya DC yasiyoridhisha hata kidogo,
kuhusu kutokuwaalika CCM, kikao kiliendelea ijapokuwa kwa hali ya kimjadala ilivyokuwa,DC pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya-DAS walionekana dhahiri kuwa ndio walikuwa wawakilishi wa CCM.

Kikao kilimalizika kwa makubaliano kwamba kila mtu akahubiri amani kwa wananchi na akawaeleze kuwa wawe watulivu kwani suala hili linashughulikiwa na haki itapatikana.

Kabla ya kikao kufungwa tulikubaliana kuwa pia ingekuwa vyema kama CCM na CHADEMA wangekutana ili pia kuhakikisha kuwa migogoro hii ya ofisi za vijiji inamalizika katika hali ambayo amani na utulivu vinakuwepo.

NAOMBA KUWASILISHA.

Evarist Ambros Silayo
Mkt-CHADEMA(W)