Serikali
imeanza kusambaza nakala milioni mbili za Katiba Inayopendekezwa nchini
kote ili kuwawezesha wananchi kuisoma na kushiriki katika Kura ya Maoni
iliyopangwa kufanyika tarehe 30 Aprili mwaka huu.
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro amesema leo (Jumatano,
Februari 11, 2015) jijini Dar es Salaam kuwa kati ya nakala hizo
zilizochapwa jijini Dar es Salaam, nakala 1,800,000 zinasambazwa
Tanzania bara na nakala 200,000 zinasambazwa Tanzania Zanzibar.
Kwa
mujibu wa Waziri Migiro, hadi kufikia jana (Jumanne, Februari 10, 2015),
jumla ya nakala 707,140 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa 12 ya
Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar ambayo imepata nakala 200,000 na kuwa
kazi hiyo inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda mfupi
ujao.
Mikoa
hiyo na nakala ziliozosambazwa katika mabano ni Katavi (15,640), Rukwa
(27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu (34,840), Mara
(52,540), Tabora (58,540) na Kigoma (41,440). Mikoa mingine ni Kagera
(54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani ambapo usambazaji
umeanza kwa wilaya ya Mafia ambayo imepata nakala 2,400.
“Idadi
ya nakala ya Katiba Inayopendekezwa kwa kila mkoa inategemea na wingi
wa kata katika mkoa, ndiyo maana baadhi ya mikoa unaona imepata nakala
nyingi,” amesema Dkt. Migiro ofisini kwake wakati akiongea na baadhi ya
waandishi wa Habari waliotaka ufafanuzi kuhusu hatua iliyofikiwa katika
kazi ya uchapishaji na uasambazaji wa nakala za Katiba Inayopendekezwa.
Kwa
mujibu wa Waziri Migiro, kuna zaidi kata 3,800 nchini kote na lengo la
Serikali ni kusambaza nakala 300 katika kila kata ambazo zitasambazwa
kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa,
Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji.
Kuhusu
taasisi za elimu na dini, Waziri Migiro amesema Serikali imepanga
kusambaza nakala 658,400 kwa taasisi za elimu, dini, vyama vya siasa na
asasi za kiraia na kuwa usambazaji huo utaanza hivi karibuni.
Pamoja
na usambazaji huo, Waziri Migiro amewakumbusha wananchi ambao bado
hawajapata nakala za Katiba Inayopendekezwa, kuisoma kupitia tovuti ya
Wizara ya Katiba na Sheria (www.sheria.go.tz) na tovuti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (www.agctz.go.tz).
Post a Comment