Wafungwa toka Thailand na Mauritius nchini wamaliza kifungo

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima
Wafungwa tisa kati ya 10 ambao Tanzania iliwapokea kutoka nchi za Thailand na Mauritius, wamemaliza kutumikia vifungo na mmoja aliyesalia kifungoni anatarajiwa kumaliza adhabu hiyo mwaka 2021.
 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alieleza bungeni jana kuwa wafungwa hao walirejeshwa kutumikia adhabu zao nchini, kufuatia Tanzania kuingia mikataba ya kubadilishana wafungwa na nchi hizo mbili.
 
Awali Ritha Kabati (Viti Maalum - CCM) alitaka kufahamishwa ni nchi ngapi ambazo Tanzania ina utaratibu wa kubadilishana wafungwa na ikiwa mataifa hayo yapo ni wafungwa wangapi wamerejeshwa nchini kupitia mpango huo.
 
Katika swali lake la nyongeza, Kabati alihoji sababu zinazozuia Tanzania kuanzisha uhusiano kama huo na  India na China, kutokana na uwepo wa raia wake wengi wanaotumikia vifungo kwa sababu mbalimbali, zikiwamo biashara ya  mihadarati.
 
Naibu Waziri Silima alisema, uhusiano wa China, India na Tanzania ni mzuri lakini ni katika mataifa ambayo raia wa Tanzania wamefanya makosa ya kisheria na kwa Afrika ni Kenya.
 
Alisema kupitia njia za diplomasia, wanaendelea kufanya taratibu za kuingia mikataba na nchi hizo, ili kufanikisha uwezekano wa kuwaruhusu wafungwa hao, kurejeshwa nchini ili kutumikia adhabu zao kwa muda utakaokuwa umebakia baada ya kusainiwa mikataba ya mahusiano ya kubadilishana wafungwa.
 
“Watu ambao wako nchi mbalimbali wanapowasiliana na balozi zetu zilizo kwenye nchi husika, wanapata misaada ya kisheria na hatuwezi kuwatelekeza isipokuwa tunatoa wito kwa wananchi wanapotaka kwenda nchi yoyote ile, kwanza wajifunze sheria za mataifa hayo” alieleza.
 
Waziri Silima alikanusha taarifa kwamba serikali imeingia mikataba ya aina hiyo na nchi hizo mbili kwasababu wafungwa wengi waliyokuwa huko ni waliyokuwa wakitumikia adhabu ya kifungo kwa kutiwa hatiani kuhusika na biashara haramu ya mihadarati.
 
Alisema hata katika nchi ambazo Tanzania haijafanikiwa kuwa na mikataba ya kubadilishana wafungwa, makosa mengi makubwa wanayokabiliwa nayo wafungwa husika ni biashara haramu ya mihadarati na kwamba jambo la msingi ni kuwapa malezi bora vijana, ili kuwaepusha na kuingia kwenye janga la biashara za madawa hayo ya kulevya.

Post a Comment

Previous Post Next Post