Prof. Muhongo: Nitazungumzia urais muda ukifika

Na Fidelis Butahe, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati makundi mbalimbali yakipigana vikumbo kumshawishi aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo agombee urais, mwenyewe amesema muda bado, ukifika atasema.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo
Baadhi ya makundi yaliyojitokeza na kumtaka agombee ni Chama cha Watu wenye ulemavu mkoani Mwanza na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Jomo Kenyatta, IAA, Semmco na Makumira.

Akiwa bungeni mjini Dodoma, Profesa Muhongo amekuwa akitajwa mara kwa mara na wabunge wenzake kama rais mtarajiwa na yeye amekuwa akifurahia kuitwa hivyo. Lakini alipoulizwa na gazeti hili kuhusu suala hilo, alijibu “Ya kwangu nitayasema muda ukifika.”

Alisema kama kuna watu wanamuunga mkono hawezi kuwazuia, ila wasiandamane kumfuata kwa nia ya kumshawishi kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.

Machi 22 mwaka huu, kupitia mwenyekiti wao, Charles Ngereza wanafunzi hao waliwaambia waandishi wa habari jijini Arusha kuwa watazunguka kwenye vyuo na taasisi zote za elimu ya juu nchini kuwashawishi wenzao kuungana nao.

“Sababu kuu ya kumuunga mkono ni rekodi ya utendaji wake. Kwa kipindi kifupi alichoongoza Wizara ya Nishati na Madini amefanya mapinduzi makubwa yaliyowashinda watangulizi wake ikiwamo kushusha bei ya kuunganisha umeme kufikia kati ya Sh27,000 hadi Sh177,000 vijijini,” alisema Ngereza.


Alisema kasi ya utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini, licha ya kuwapatia wananchi huduma ya nishati, pia imechangamsha uchumi kwa kuongeza shughuli za uzalishaji zinazotegemea nishati ya umeme.

Muhongo: Ni mapema mno

Profesa Muhongo alisema kuwa ni mapema sana kuzungumza kama atawania urais au la.

“Hawajaja (wanafunzi) kuniona kama wanataka (kunishawishi) waendelee huko huko si kuja kwangu,” alisema.

Aliongeza, “Taratibu zimewekwa mbona mnakuwa na wasiwasi, ya kwangu nataka nikiyaongea muda uwe umefika.”

Katika hoja zao wanafunzi hao, walisema hatua ya Profesa Muhongo kujiuzulu ilitokana na uwajibikaji kutokana na dhamana aliyokuwa nayo.

Walisema hiyo ni moja ya sifa za uongozi na kumtaja Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi aliyejiuzulu uwaziri wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na baadaye kuukwaa urais.

Wanafunzi waliohudhuria mkutano huo na vyuo vyao kwenye mabano ni Rahma Sengela (Jomo Kenyatta), Daudi Shayo (IAA), Sarah Aminarabi (Arusha), Nelson Machumu (Semmco) na Hobeshi Juvenary kutoka Makumira.

Chanzo: Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم