WAKATI timu za Tanzania zikiwa zimezoea kucheza kwa ratiba laini
ya mechi moja kwa wiki, Simba sasa inaonekana kupata kiburi baada ya
kusema kuwa ratiba mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo kwa
maelezo ya awali imedai kuwa kutakuwa na mechi siku za wikiendi na
katikati ya wiki, kwao ni bab’kubwa na itawabeba mbele ya wapinzani wao
Yanga na Azam.
Pia kocha, Dylan Kerr, ametoa mpya baada ya kusema
kwamba anataka kuunda kikosi cha wachezaji 25, lakini kwenye mchezo
mmoja hata akibadilisha wachezaji watano ubora uwe uleule.
Timu nyingi za hapa nchini ikiwemo Yanga na Azam
mara kadhaa zimekuwa zikilalamikia ratiba ya kucheza mechi nne ndani ya
wiki mbili kuwa ni ngumu jambo ambalo kocha wa Kerr amelipinga vikali
akisema hilo ndiyo soka la kisasa.
TFF imesogeza mbele kuanza kwa michuano ya Ligi
Kuu Bara hadi Septemba 12 ambapo pia miongoni mwa mikakati yao katika
ratiba mpya inayofanyiwa marekebisho ni kuweka mechi kila wikiendi na
katikati ya wiki.
Kerr alisema kama ratiba itakuwa hivyo itambeba
kwani anatengeneza kikosi imara ambacho kitaweza kupata matokeo katika
mechi za mfululizo.
Kocha huyo raia wa Uingereza alisema atatengeneza
wachezaji kati ya 22 na 25 ambao watakuwa fiti kucheza wakati wowote ili
ratiba hiyo isimpe shida.
“Ni uamuzi sahihi kuweka mechi mbili kwa wiki,
wachezaji watakuwa imara maana kama wanacheza mara moja kwa wiki na
kupumzika kwa siku nyingine saba siyo jambo zuri hasa kwa viwango vyao,”
alisema.
“Kwangu nadhani itakuwa ni ratiba nzuri,
nitatengeneza kikosi ambacho kitaweza kuhimili mikiki mikiki ya mechi
hizo na kutupatia matokeo stahiki.
“Nataka kuwa na wachezaji kati ya 22 na 25 ambao
watakuwa fiti kucheza kwa wakati wowote, hata tukifanya mabadiliko ya
wachezaji wanne hadi watano katika kikosi kilichocheza mechi ya mwisho
tunakuwa na uhakika wa ushindi.
“Ila sitakuwa nafanya mabadiliko bila sababu za
msingi, kikosi bora ndicho kitakachocheza hata kama kilitoka kucheza
siku tatu nyuma.”
Wakati huo huo kocha huyo amesema wameanza rasmi
mazoezi makali ya kucheza mpira kwenye kambi yao ya visiwani Zanzibar
ambapo jana Jumatano walitumia zaidi ya saa nne katika mazoezi hayo
asubuhi pamoja na jioni.
Kerr alisema licha ya kwamba bado wanafanya
mazoezi ya viungo na utimamu wa mwili, kambi yao ya Zanzibar imejikita
zaidi katika kucheza mpira ikiwemo kuwapa wachezaji wake mbinu kadhaa za
mchezo.

Post a Comment