TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tumewaita kuwaomba mtusaidie kufikisha ujumbe ufuatao kwa Watanzania:
MWENENDO WA KAMPENI ZA CCM
Hadi
jana, tarehe 16 September 2015, Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe
Magufuli, alikuwa amekwishafanya kampeni katika mikoa 12 na Majimbo 94.
Amekwishafanya mikutano mikubwa ya hadhara 76 na mikutano ya barabarani
381. Amekwishatembea, kwa gari, jumla ya kilomita 13,720. Kwa ujumla
amekwishakutana, moja kwa moja, na asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura.
Kwa kuwa baadhi ya mikutano yetu inatangazwa moja kwa moja na redio za
kijamii na luninga, wapiga kura waliopata nafasi ya kumsikia
wanakadiriwa kufikia asilimia 70.
Tunafarijika
na idadi kubwa ya watu wanaokuja kwenye mikutano ya kampeni zetu.
Tunafarijika pia kwamba karibu Watanzania wote wanaopata fursa ya
kumuona na kumsikia wamemuelewa na wamepata matumaini ya Tanzania Mpya
kupitia kwake. Utafiti wetu wa ndani, tulioufanya kwa kipindi cha siku
kumi zilizopita katika majimbo 246 kati ya majimbo 269, unaonyesha
kwamba Dr. Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3 Tunaamini kwamba
asilimia hizi zitaongezek kadri Watanzania wengi zaidi wanavyopata fursa
ya kumsikiliza Dr. Magufuli na kusikiliza Ilani na sera za CCM.
Kwa
upande wa kampeni zetu za Ubunge, zaidi ya robo tatu ya wagombea Ubunge
wa CCM wamekwishazindua kampeni zao na wanaendelea vizuri. Sekretarieti
ya Kampeni ya CCM inaanda program maalum ya kampeni katika majimbo
yenye changamoto mahsusi.
Napenda
kuchukua fursa hii kuwajulisha wana-CCM kwamba viongozi na makada
wengine wa CCM, waliopo madarakani na wastaafu watapita tena, jimbo kwa
jimbo, nchi nzima katika siku 30 za mwisho katika jitihada za kuongeza
ushindi wa CCM na Dr. Magufuli.
MIDAHALO YA WAGOMBEA
Wiki
tatu zilizopita, CCM, na kwa hakika vyama vingine pia, ilipokea mwaliko
wa Mgombea Urais wa CCM, Dr. John Pombe Magufuli, kushiriki kwenye
mdahalo wa wagombea Urais uliondaliwa na Baraza la Habari Tanzania
(Media Council of Tanzania) kwa kushirikiana na taasisi nyingine kadhaa,
ikiwemo Twaweza. Dr. Magufuli amekubali kushiriki katika mdahalo huo.
Kwa msingi huo, kauli ya UKAWA iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, Ndugu James Mbatia, kwamba UKAWA inaomba mdahalo ni njia
ya kuwahadaa Watanzania tu kwa kuwa mwaliko wa mdahalo ulikwishatolewa
mapema kwa vyama vyote na wanaotakiwa kushiriki ni wagombea Urais wa
vyama.
CCM
inafurahishwa na utamaduni wa midahalo ambao unaanza kujitokeza katika
chaguzi zetu. Na inaamini kwamba midahalo ya Wagombea Urais ni
sehemu
muhimu ya kuwashirikisha wapiga kura katika mchakato wa uchaguzi na
kuwasaidia waamue nani wamchague kwa misingi ya hoja na sera na sio kwa
ushabiki, kwa mihemko, na kwa propaganda. Mdahalo unatoa fursa ya
wagombea kuulizwa maswali ya moja kwa moja na kutoa ufafanuzi wa kina
kuhusu sera na ahadi zao, fursa ambayo hawaipati kwenye mikutano ya
hadhara kampeni.
Hatukubaliani
na kauli ya UKAWA kwamba mdahalo usiwe baina ya wagombea bali uwe baina
ya Wenyeviti wa Vyama. Tunaamini hoja hii ni kichekesho. Haijawahi
kutokea popote duniani kwenye utamaduni wa midahalo, kwamba wagombea
wasishiriki bali watu wengine ndio wafanye midahalo kwa niaba yao.
Tunaamini mdahalo huu unapaswa kuwa baina ya wagombea. Wao ndio
wanaoomba dhamana. Wao ndio wanaopaswa kujibu maswali na kufafanua
kuhusu ahadi zao.
CCM
inaamini kwamba ili mdahalo huu uwe na tija, wagombea Urais wote, hasa
wa vyama vikuu, wawepo na washiriki. Mdahalo hautakuwa na maana
kama mgombea mmojawapo wa vyama vikuu atatengeneza kisingizio ili asishiriki.
UCHAGUZI WA AMANI
CCM
inasikitishwa na kauli zinatolewa na baadhi ya viongozi wa UKAWA zenye
kuashiria fujo na vurugu. Kauli kwamba kura zitaibiwa hazina msingi
wowote. Kauli hizi zinaashiria maandalizi ya kushindwa na maandalizi ya
kufanya vurugu baada ya matokeo ya kushindwa.
Utaratibu
wa uchaguzi wetu unajulikana na umekubalika na vyama vyote. Kura
zinapigwa kituoni na kuhesabiwa kituoni mbele ya mawakala wa vyama
vyote, wasimamizi wa uchaguzi na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje
ya nchi. Baada ya kura kuhesabiwa, matokeo yanajazwa katika fomu ambayo
kila wakala anasaini na kupewa nakala. Nakala ya matokeo hayo pia
inabandikwa nje ya kituo cha kupiga kura. Kila Chama, na kila Mtanzania,
kina fursa ya kujumlisha matokeo yake kwenye kila kituo na kupata jumla
kuu. Matokeo ya nchi nzima yanajumlishwa mahala pamoja huku kukiwa na
waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi, pamoja na wawakilishi wa
vyama vyote na wao wakiwa na fomu zao za kila kituo nchi nzima.
Tunapenda
kuwasihi Watanzania wasikubali vishawishi vya kufanya vurugu. Mara
nyingi, viongozi wanaohamasisha vurugu wanakuwa na ulinzi au walinzi au
uwezo wa kukimbilia pahala penye utulivu zaidi huku wakiwaacha wafuasi
wao katika wakihangaika.
UCHAGUZI NA UMOJA WA KITAIFA
CCM
pia inapenda kusisitiza imani yake kwamba uchaguzi haupaswi kutugawa
kama taifa. Uchaguzi ni tukio la kupita. Kuna maisha baada ya uchaguzi.
Kuna taifa baada ya uchaguzi. Lazima taifa liendelee kubaki moja,
tuendelee kubaki wamoja. Tusitoe kauli za kupitiliza zenye mrengo wa
kujenga chuki katika jamii na kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu.
Kama
Chama kilichoasisi umoja wa taifa letu, tunaendelea kuasa kwamba
wanasiasa wasijinadi kwa misingi ya udini, ukabila wala ukanda. CCM
haina mpango kuendeleza mjadala wa kauli ya Mgombea wa UKAWA Ndugu
Edward Lowassa aliyoitoa kanisani Tabora tarehe 6 September 2015
kwamba
nchi ilishapata viongozi Wakatoliki na kwamba sasa ni zamu ya Walutheri
kuchukua nafasi hiyo. Tunaamini mjadala huo hauna tija. Tunaamini
kwamba Watanzania wengi, wa dini na madhehebu yote, hawaamini katika
siasa za namna hii. Tuliamini kwamba UKAWA ingetumia fursa ya mkutano
wao na waandishi wa habari jana kuomba radhi kwa Watanzania. Kwakuwa
hawakufanya hivyo, tunapendekeza mjadala wa jambo hili ufungwe. Itoshe
tu kwamba Ndugu Lowassa amesema hivyo, Tume ya Uchaguzi imemuonya, na
yeye hajajitokeza kuomba radhi wala kufafanua. Watanzania wamemjua ni
kiongozi wa aina gani na watatoa hukumu yao tarehe 25 Oktoba 2015.
Imetolewa na:-
January Y. Makamba,
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM
MJUMBE WA KAMATI YA KAMPENI YA CCM
16/9/2015
إرسال تعليق