Mkuu wa Upelelezi TANAPA achinjwa Kinyama


POLISI mkoani Arusha imewatia mbaroni watu wawili wanaohusishwa na tukio la kuuawa kinyama kwa kuchinjwa shingo kwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Stephen Kisamo.
Kifo cha Kisamo kinahusishwa na mambo mengi yakiwemo vita ya kupambana na ujangili, ikielezwa mkuu huyo alikuwa na siri nzito juu ya watu wanaojihusisha na ujangili wakiwemo wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Arusha, watumishi wa serikali na wanasiasa.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Arusha zilieleza tayari imewatia ndani watu wawili ambao ni marafiki wakubwa wa Kisamo na wanajua siri nzito kutokana na kunaswa kwa mawasiliano ya simu ya kiganjani kati ya marehemu na watu fulani muda mfupi kabla ya mauti kumfika ambao polisi inawachunguza kwa karibu.
“Wasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas sisi tumeshakamata watu wawili wa karibu na marehemu na sms na mawasiliano yanatia shaka, lakini ukweli utajulikana muda si mrefu,” kilieleza chanzo chetu cha habari ndani ya Jeshi la Polisi.
Kamanda Sabas alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo Desemba 18, mwaka huu asubuhi katika eneo la Kikwakwaru jijini Arusha muda mfupi baada ya Kisamo kutoka nyumbani kwake akiwa na gari aina ya Mazda.
Sabas alisema siku hiyo hiyo jioni alifika kituoni hapo mke wa marehemu na kueleza juu ya kutoweka kwa mumewe ambapo mara moja polisi walianza kufuatilia jambo hilo bila mafanikio.
Kamanda Sabas alisema usiku, Polisi ilipokea taarifa kutoka kwa raia wema wa eneo hilo la Kikwakwaru kuhusu kuonekana kwa gari hilo likiwa limeegeshwa maeneo hayo kwa muda mrefu bila kuonekana mtu yeyote ambapo walifika na kulikuta gari hilo, lililovutwa hadi katika Kituo Kikuu cha Polisi usiku huo na baadaye lilitambuliwa na mke wa Kisamo.
Baadaye walirejea eneo la tukio kwa lengo la kutafuta mwili wa marehemu huyo, lakini hawakufanikiwa kuupata mwili wala kumuona kachero huyo ambapo walilazimika kuomba ruhusa ya kupekua gari hilo.
Alisema baada ya kuomba ruhusa hiyo, mke wa marehemu alipowasilisha ufunguo wa akiba wa gari na Polisi walipofungua na kuanza upekuzi walikuta mwili wa marehemu ukiwa umekunjwa kwenye buti, huku shingo yake ikiwa imechinjwa eneo la nyuma ya shingo yake.
Aidha, Kamanda Sabas alisema kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, mumewe alikuwa mgonjwa na alikuwa akijiandaa kwa safari ya India kwa matibabu, hivyo kabla ya tukio walidhani alitekeleza gari baada ya kuzidiwa na ugonjwa.
Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru

Post a Comment

Previous Post Next Post