SAKATA la mabilioni ya
fedha zenye utata zinazodaiwa kuwa ni za Watanzania zilizofichwa katika
baadhi ya benki za nchini Uswisi, limeingia katika sura mpya, ikibainika
ya kwamba kwa sasa wanaodaiwa kuwa na akaunti hizo ni lazima watoe
idhini ya kukaguliwa kwa taarifa zao za kibenki.
Fedha hizo takriban Sh.
bilioni 303.7 zinadaiwa kufichwa na baadhi ya viongozi nchini Uswisi,
wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa.
Tayari Bunge
limekwishatoa maelekezo kwa serikali kufuatilia sakata hilo na
kuwasilisha taarifa yake katika mkutano wa Bunge wa Aprili, mwaka huu,
huku viongozi mbalimbali nchini wakitoa kauli za kukinzana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-Utawala Bora, George Mkuchika, kwa upande wake, mara kwa mara
amekuwa akiwataka viongozi wanaodai kuwajua waliotunza fedha hizo
wawataje kwa majina, lakini wengi wakimkosoa na kutaka Serikali itimize
wajibu wake katika suala hilo.
Safari hii, akizungumzia
mchakato wa kuzirejesha fedha hizo katika mahojiano yake na mwandishi
wetu hivi karibuni, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu,
anakiri ugumu wa kurejesha fedha hizo na kueleza kwamba mchakato wa
kuzirejesha utahitaji pia taarifa kutoka kwa wenye fedha hizo.
“Kitu kikubwa katika
hili ni kwamba Serikali kwa sasa iko katika mchakato wa kulifanyia kazi
suala hili. Ninachoweza kusema kiujumla, ziko ripoti za kimataifa
zinazotolewa kila mwaka kwa nchi zote, zinazoeleza ni watu wa taifa gani
wanaweka fedha katika taifa gani.
“Kwa mfano, Uswisi
inatoa ripoti hii kila mwaka, na Marekani inatoa ripoti yake kila mwaka,
inayosema wakazi wa Tanzania, katika akaunti za benki za nchi ile
wanaweza kuwa wameweka kiasi fulani cha fedha katika akaunti zao.
“Lakini benki hizo,
chini ya sheria zao, huwa hawataji (mteja wao) mmoja mmoja, wakisema
huyu ana kiasi hiki, huyu ana kiasi kile…inaitwa ‘confidentiality law.’
Wao (Uswisi) wamekuwa kivutio kikubwa kwa watu kuweka fedha zao huko kwa
sababu hawatoi siri za wateja wao.
“Kwa hiyo, itatubidi
tufanye kazi ya ziada kuzipata, hata hiyo ya kusema tunaifanyia kazi,
wenyewe wale wenye akaunti zao kule ni mpaka wao wakubali kutoa taarifa
zao, na ujue kwamba wakikubali wenyewe watakuwa wameharibu msingi wa
biashara yao. Kwa hiyo, changamoto zipo.
“Tunafanyia kazi, lakini
changamoto ya kupata taarifa za mtu mmoja mmoja, tukubali hizi zipo,”
anasema Gavana Ndulu katika mahojiano yaliyochapishwa ndani ya toleo
hili.
Sakata hilo la mabilioni
ya Uswisi liliwasilishwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe
Zitto na kuwekewa azimio la Bunge la kuitaka Serikali kufuatilia suala
hilo na kurejesha ripoti yake bungeni.
Kati ya viongozi wengine
walionukuliwa kuzungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti, ni pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, na Balozi wa
Uswisi nchini, Olivier Chave, ambaye amepata kunuliwa akisema Serikali
haijaonyesha nia ya kufuatilia sakata hilo.
Katika maelezo yake, Jaji Werema alinukuliwa akisema Serikali inaendelea kufuatilia suala hilo na tayari imeundwa timu maalumu.
Kwa mujibu wa Werema,
timu hiyo maalumu iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye
alifanya hivyo kutokana na idhini ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba, timu
hiyo itakuwa ikifanya kazi zake kwa siri.
Hata hivyo, katika
msisitizo wake bungeni mwaka jana, Zitto Kabwe, alidai kuwa na orodha
ya majina 10 ya vigogo serikalini na wastaafu ambao ndio wamiliki wa
fedha hizo.
Miongoni mwao anatajwa
kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni
wabunge hadi sasa, na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu
Tanzania (BoT).
Kwa mujibu wa Zitto,
katika orodha ambayo Waziri wa Fedha wa Ufaransa anayo, kuna Watanzania
lakini akaituhumu Serikali akisema haitaki kufuata njia halali za kupata
orodha hiyo kwa kuwa viongozi wengi na wafanyabiashara wakubwa wana
akaunti katika benki za Uswisi.
source: Raia Mwema
Post a Comment