Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mh. Ban Ki Moon akiwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. (Picha na Maktaba).
KATIBU Mkuu
wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon amempongeza na
kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete kwa kutoa mapendekezo muhimu na murua ya aina yake ya
kuanza kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Maziwa Makuu kwa njia ya
mazungumzo badala ya kutegemea mapambano ya silaha peke yake.
Aidha,
Katbu Mkuu huyo wa UN ameishukuru Tanzania kwa kuchangia askari wa
kuunda Brigedi Maalum ya Kusimamia Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Congo (DRC) na pia kutoa kamanda wa Brigedi hiyo.
Vile vile,
Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwomba Rais Kikwete kuendelea kuunga mkono
jitihada za kuleta amani na utulivu katika DRC na eneo lote la maziwa
makuu kupitia Mchakato wa Kanda wa Kusimamia Amani (Regional Oversight Mechanism) katika eneo hilo.
Mheshimiwa
Ban Ki Moon ametoa shukrani na pongezi hizo kwa Rais Kikwete wakati
viongozi hao walipokutana leo, Jumapili, Juni 2, 2013, kwa mazungumzo
wakati wa Mkutano wa Tano wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD V)
unaoendelea mjini Yokohama, Japan.
Wakati wa
mazungumzo hayo kwenye Hoteli ya Intercontinental ambako viongozi hao
wamefikia, Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwambia Rais Kikwete: “Nakushukuru
sana Mheshimiwa Rais kwa mchango wako mzuri kwenye mkutano wetu wa
Jumapili asubuhi mjini Addis Ababa. Yako yalikuwa mapendekezo bora zaidi
na mapya katika mkutano wetu mzuri. Asante sana kwa kuunga mkono
Mchakato wa Kanda wa Kusimamia Amani katika eneo la Maziwa Makuu.
Tunaomba uendeleaa kuunga mkono Mchakato huu.”
Ameongeza Katibu Mkuu wa UN: “Nilipokuwa
Goma karibuni nilikutana na Jenerali kutoka Tanzania ambaye ni Kamanda
wa Brigedi Maalum ya Kulinda Amani katika DRC iliyoko chini ya Umoja wa
Mataifa. Tunakushukuru sana kwa kuchangia Brigedi hii na tunakushukuru
sana kwa kukubali kutoa Kamanda wa Brigedi hii.”
Katibu Mkuu
Ban Ki Moon pia amemwalika Rais Kikwete kushiriki katika kikao kijacho
cha Mchakato kilichopangwa kufanyika kwenye Umoja wa Mataifa Septemba
mwaka huu wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mwaka
huu.
“Nakusudia
kuitisha kikao kingine cha Mchakato wetu katika wiki kati ya Septemba
20 na 27, mwaka huu, 2013 wakatiwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na
napenda kukualika ushiriki katika kikao hiki muhimu sana katika jitihada
zetu za kuleta amani katika eneo la Maziwa Makuu na hasa katika Congo,” Mheshimiwa Ban Ki Moon amemwambia Rais Kikwete.
Rais
Kikwete amemwambia Katibu Mkuu wa UN kuwa anaendelea kuamini kuwa
matumizi ya nguvu za kijeshi na askari peke yake hayataweza kuleta amani
katika eneo la Maziwa Makuu ikiwamo DRC. “Huu ndio msimamo ambao
niliueleza katika mkutano ule wa Jumapili iliyopita mjini Addis Ababa
hata kama baadhi ya watu hawakufurahishwa sana na msimamo huu.”
“Tumekuwa
tunajaribu kutumia nguvu kuleta amani katika DRC tokea mwaka 1997 na
bado mpaka sasa hatujafanikiwa kuleta amani ya kudumu katika nchi hii
jirani – tokea wakati huo tumejaribu kuunga mkono uasi mmoja baada ya
mwingine lakini bado tuko pale pale na ndiyo maana naamini kuwa wakati
umefika wa kuelekeza nguvu zetu katika mazungumzo ya hatua tatu kama
nilivyoelekeza katika mkutano ule wa wiki iliyopita.”
Viongozi
hao wawili pia wamejadili hali ilivyo katika Madagascar na maandalizi ya
uchaguzi mkuu nchini humo. Aidha, viongozi hao wawili walijadili
maendeleo ya kisiasa katika Zimbabwe ambako Katibu Mpya imepitishwa na
sasa maandalizi yanafanywa kwa ajili ya uchaguzi mkuu nchini humo.
Rais
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya
Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ametoa ufafanuzi wa ndani
kuhusu jitihada ambazo zimekuwa zinafanywa na Asasi yake kuhusu suala
la Madagascar baada ya kuwa ameombwa na Mheshimiwa Ban Ki Moon kuhusu
jitihada hizo.
Rais
Kikwete amemwambia Mheshimiwa Ban Ki Moon kuwa viongozi wa SADC
watakutana mjini Maputo, Mozambique wiki ijayo kujadili matukio ya
karibuni katika Madagascar na maendeleo ya kisissa katika Zimbabwe.
Mapema leo,
Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uchumi,
Biashara na Viwanda (METI) wa Japan Mheshimiwa Toshimitsu Motegi.
Katika
mkutano huo, Mheshimiwa Motegi ameomba Serikali ya Tanzania kuyasaidia
makampuni ya Japan ambayo yanajaribu kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
2 Juni, 2013
Post a Comment