UCHAGUZI MDOGO TPLB NOVEMBA 15
Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) utafanyika Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo moja ya ajenda ni uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi moja ya uongozi kwenye bodi hiyo.
Nafasi hiyo ya ujumbe kwenye
Kamati ya Uendeshaji ya TPLB iliyokuwa ikishikiliwa na Kazimoto Muzo
imebaki wazi baada ya klabu yake ya Pamba ya Mwanza kushuka daraja
kutoka la Kwanza hadi la Pili.
Hivyo, wagombea wa nafasi hiyo ni
kutoka kwenye klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Klabu hizo zina
nafasi mbili kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB ambapo nyingine
inashikiliwa na Omari Mwindadi wa klabu ya Mwadui ya Shinyanga.
SDL WAONGEZEWA MUDA WA USAJILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili wa wachezaji kwa timu za Ligi
Daraja la Pili (SDL) kwa siku saba ambapo sasa utamalizika Oktoba 21
mwaka huu.
Awali usajili huo unaofanyika kwa
njia ya mtandao (online) ulikuwa umalizike jana (Oktoba 14 mwaka huu),
lakini ni klabu chache ndizo zilizoweza kusajili ndani ya muda
uliopangwa.
Klabu ambazo hazijakamilisha
shughuli hiyo ya usajili, zinatakuwa kukamilisha ndani ya siku hizo saba
kwani TFF haitaongeza tena muda wa usajili. Vilevile klabu za SDL
zinakumbushwa kuwasilisha majina ya viwanja vya nyumbani ambavyo timu
zao zitatumia kwenye ligi hiyo.
TFF ilifanya mafunzo ya usajili kwa maofisa usajili wa klabu hizo Oktoba 6 na 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Timu za SDL zimegawanywa katika
makundi manne ya timu sita zitakazocheza ligi kwa mtindo wa nyumbani na
ugenini. Kundi A lina timu za Mpanda United ya Katavi, Ujenzi (Rukwa),
Mvuvumwa FC (Kigoma), Mji Mkuu FC (Dodoma), Milambo (Tabora) na Singida
United (Singida).
Kundi B ni Mbao FC (Mwanza),
Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), JKT Rwamkoma (Mara),
Pamba (Mwanza) na AFC (Arusha). Kundi C ni Navy, Mshikamano, Transit
Camp na Abajalo za Dar es Salaam, Kiluvya United (Pwani) na Kariakoo
(Lindi(.
Timu zinazounda kundi D ni
Magereza (Iringa), Town Small Boys (Ruvuma), Njombe Mji (Njombe),
Volcano FC (Morogoro), Wenda FC (Mbeya) na Mkamba Rangers (Morogoro).
MAREKEBISHO YA RATIBA FDL KUNDI A
Mechi nne za Kundi A la Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) zimefanyiwa marekebisho ili kutoa fursa ya
matumizi ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Timu za African Lyon na Kimondo FC
ambazo awali zilikuwa zicheze Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa
Mabatini mkoani Pwani, sasa zitacheza Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa
Karume, Dar es Salaam.
Nayo mechi ya Polisi Dar es Salaam
na Majimaji ya Songea iliyokuwa ichezwe Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa
Karume, Dar es Salaam, sasa itachezwa Oktoba 27 mwaka huu kwenye uwanja
huo huo.
Mechi ya Friends Rangers na
Ashanti United iliyokuwa ichezwe Mabatini mkoani Pwani, Oktoba 26 mwaka
huu, sasa itachezwa Uwanja wa Karume, Oktoba 28 mwaka huu.
Pia mechi ya Lipuli FC na JKT
Mlale iliyokuwa ichezwe Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Samora
mjini Iringa, imesogezwa mbele kwa siku moja. Mechi hiyo sasa itachezwa
Oktoba 26 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Post a Comment